KLABU Bingwa ya Afrika Mashariki na Kati, Azam FC, muda wowote kuanzia sasa itaanza safari ya kuelekea mkoani Pwani tayari kabisa kuikabili Ruvu Shooting katika mchezo wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara (VPL) utakaofanyika Uwanja wa Mabatini kesho Alhamisi saa 10.00 jioni.

Kikosi hicho kinaelekea huko na nyota wake 20, ambao watakuwa na kazi moja tu ya kuhakikisha wanasaka ushindi muhimu ili kujiweka sawa kwenye msimamo wa ligi hiyo, ambapo kwa sasa imejizolea pointi 45 katika nafasi ya tatu nyuma ya Yanga na Simba zilizo juu yake.

Akizungumza na mtandao rasmi wa klabu www.azamfc.co.tz Kocha Msaidizi wa Azam FC, Idd Nassor Cheche, ameweka wazi kuwa watautumia mchezo huo kama sehemu ya kuwapa furaha mashabiki wao kwa kuibuka na ushindi na kuzoa pointi zote tatu.

“Mashabiki waje kwa wingi kutupa sapoti, sisi hatutawaangusha tutawapa kile wanachotarajia kwa kuibuka na ushindi dhidi ya Ruvu Shooting, tunajua mchezo utakuwa mgumu lakini tumejipanga kukabiliana na hilo,” alisema.

Kikosi hicho kinaondoka huku kikiwa kimeimarishwa na urejeo wa washambuliaji wake wawili, Mbaraka Yusuph na Bernard Arthur, ambao hivi sasa wako fiti baada ya kupona majeraha yaliyokuwa yakiwakabili.

Aidha, Azam FC itaimrishwa kwenye eneo la beki wa kushoto kwa urejeo wa Bruce Kangwa, ambaye aliukosa mchezo uliopita dhidi ya Mbeya City kutokana na kutumikia adhabu ya kukosa mechi moja baada ya kukusanya kadi tatu za njano.

Lakini itaendelea kuwakosa mabeki wake, Yakubu Mohammed, Daniel Amoah, David Mwantika na washambuliaji Shaaban Idd, ambao bado ni wagonjwa huku mshambuliaji Wazir Junior, akiwa tayari ameanza mazoezi na wenzake jana baada ya kumaliza siku tano za mapumziko za kumalizia matibabu ya kifundo cha mguu.

Wachezaji wanaosafiri ni makipa, Mwadini Ally, Razak Abalora, mabeki Nahodha Msaidizi, Agrey Moris, Bruce Kangwa, Abdallah Kheri, Swaleh Abdallah, Lusajo Mwaikenda, viungo ni Nahodha Himid Mao ‘Ninja’, Salum Abubakar ‘Sure Boy’, Frank Domayo ‘Chumvi’, Salmin Hoza, Braison Raphael, Masoud Abdallah.

Mawinga ni Idd Kipagwile, Ramadhan Singano ‘Messi’, Joseph Mahundi, Enock Atta, huku washambuliaji wakiwa ni Mbaraka Yusuph, Yahya Zayd na Bernard Arthur.