KLABU Bingwa ya Afrika Mashariki na Kati, Azam FC, imetoka suluhu dhidi ya Mbeya City katika mchezo wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara (VPL) uliomalizika kwenye Uwanja wa Sokoine jijini Mbeya leo jioni.

Matokeo hayo yanaifanya Azam FC kufikisha jumla ya pointi 45 kwenye msimamo wa ligi hiyo ikiwa imebakia nafasi ya tatu, ikizidiwa pointi nne na kinara Simba aliyenazo 49 na Yanga ikiwa imejikusanyia 46 katika nafasi ya pili, timu hizo mbili zikiwa na mechi mbili mkononi.

Azam FC ilianza vema mchezo huo ikitengeneza nafasi kadhaa za kufunga lakini umakini ulionekana kukosekana kwenye eneo la umaliziaji, moja ya nafasi ni ile iliyopotezwa na mshambuliaji Shaaban Idd, aliyemfinya beki na kupiga shuti lililopanguliwa na kipa kabla ya mpira huo kumgonga kiungo Frank Domayo na kudakwa tena na kipa Owen Chaima.

Mshambuliaji wa Azam FC, Yahya Zayd, alifanya kazi ya ziada dakika ya 11 baada ya kuwatoka mabeki wa Mbeya City na kupiga shuti kali nje ya eneo la 18 lililopanguliwa na kipa kabla ya kuuwahi mpira na kuudaka tena.

Kwa muda mrefu wa mchezo huo, timu zote zilikuwa zikishambuliana kwa zamu huku safu ya ulinzi ya Mbeya City ikionekana kufanya kazi ya ziada kuwazuia washambuliaji wa Azam FC, Zayd na Shaaban, ambao walikuwa wamepewa ulinzi mkali leo kila walipokuwa wakigusa mpira.

Mabadiliko ya kipindi cha pili kwa nyakati tofauti ya benchi la ufundi la Azam FC la kuwaingiza winga Idd Kipagwile, mshambuliaji Joseph Kimwaga na kiungo Braison Raphael, yaliongeza ari ya kikosi hicho kwenda kusaka bao la ushindi lakini Mbeya City ilisimama vema kuondoa hatari zote huku pia wakionekana kupoteza sana muda dakika za mwishoni.

Wakati mchezo huo ukielekea ukingoni, mshambuliaji Shaaban Idd, alilazimika kukimbizwa Hospitali ya Rufaa ya mkoa wa Mbeya baada ya kudondoka alipofanyiwa mabadiliko kuingia Kimwaga, hii ni kufuatia kifua kumbana ghafla kutokana na hali ya ubaridi ya mkoani humo.

Shaaban anaendelea vizuri hivi sasa akiwa anamalizia taratibu za matibabu kabla ya kuruhusiwa kuondoka hospitalini hapo.

Kikosi cha Azam FC kinatarajia kuondoka jijini Mbeya kesho Jumatatu alfajiri tayari kurejea Dar es Salaam kujiandaa na mchezo ujao wa ligi dhidi ya Ruvu Shooting utakaofanyika Uwanja wa Mabatini mkoani Pwani Alhamisi ijayo.

Kikosi cha Azam FC:

Razak Abalora, Swaleh Abdallah, Salmin Hoza, Abdallah Kheri, Agrey Moris, Himid Mao (C), Salum Abubakar, Frank Domayo/Braison Raphael dk 72, Shaaban Idd/Joseph Kimwaga dk 84, Yahya Zayd, Joseph Mahundi/Idd Kipagwile dk 66