KLABU Bingwa ya Afrika Mashariki na Kati, Azam FC, itakuwa kibaruani ugenini kutafuta pointi tatu muhimu pale itakapokuwa ikikabiliana na Mbeya City kwenye Uwanja wa Sokoine, jijini Mbeya kesho Jumapili saa 10.00 jioni.

Tayari kikosi cha Azam FC kimeshawasili mkoani humo jana usiku baada ya safari ndefu ya takribani saa 17 ikitokea jijini Dar es Salaam, ambapo imejidhatiti vilivyo kupata ushindi na leo jioni kitafanya mazoezi ya mwisho kwenye uwanja huo.

Benchi la ufundi la timu hiyo chini ya Mromania, Aristica Cioaba, limeweka mikakati ya kumaliza vema mechi nane zilizobakia za Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara (VPL) kwa kuanza na mchezo huo ili kujiweka sawa kwenye msimamo wa ligi hiyo.

Azam FC itaingia dimbani ikiwa na kumbukumbu ya kupoteza mchezo wa Kombe la Shirikisho (Azam Sports Federation Cup) dhidi ya Mtibwa Sugar, lakini imefanya vema kwenye mechi tatu zilizopita za ligi baada ya kushinda zote ikizichapa Mwadui (1-0), Singida United (1-0) na Mbao (2-1).

Matajiri hao kutoka viunga vya Azam Complex watakuwa bila nyota wake sita ambao ni wagonjwa, Yakubu Mohammed ambaye tayari ameshatolewa hogo ‘P.O.P’, Daniel Amoah, David Mwantika, wakiwa wagonjwa huku washambuliaji Mbaraka Yusuph, Bernard Arthur, Wazir Junior wakimalizia programu ya mwisho ya kurejea uwanjani baada ya kupona majeraha.

Aidha pia Azam FC itamkosa beki wa kushoto, Bruce Kangwa, atakayesimama kucheza mechi moja baada ya kukusanya kadi tatu za njano.

Timu hizo zilipokutana kwenye mchezo wa mzunguko wa kwanza iliyofanyika Uwanja wa Azam Complex, Azam FC ilishinda bao 1-0 lililofungwa na mshambuliaji Mbaraka Yusuph

Hadi sasa kwenye msimamo wa ligi hiyo, Azam FC inayodhaminiwa na Benki ya NMB, Maji safi ya Uhai Drinking Water na Tradegents, inashika nafasi ya tatu ikiwa na pointi 44 ikizidiwa pointi mbili na Yanga iliyo nafasi ya pili kwa pointi 46 huku Simba ikiwa kileleni kwa pointi 49, timu hizo mbili za juu zikiwa na mchezo mmoja mkononi kila mmoja.