BENCHI la Utabibu la Klabu Bingwa ya Afrika Mashariki na Kati, Azam FC, limetoa ripoti ya maendeleo ya wachezaji wawili wa timu hiyo, mshambuliaji Wazir Junior na beki Daniel Amoah, waliopelekwa kwenye Hospitali ya Vincent Pallotti jijini Cape Town, Afrika Kusini kwa matibabu.

Wakati Junior akiwa anasumbuliwa kwenye enka, Amoah kwa upande wake alikuwa akisikia maumivu kwenye goti, majeraha aliyopata miezi miwili iliyopita katika mchezo wa kirafiki wa Azam FC dhidi ya Polisi Tanzania baada ya kudondokea sakafu nje ya uwanja.

Daktari Mkuu wa Azam FC, Dr. Mwanandi Mwankemwa, ameuambia mtandao rasmi wa klabu www.azamfc.co.tz kuwa Amoah amekutwa na tatizo kubwa kwenye goti lake na atafanyiwa upasuaji Alhamisi hii na atalazimika kukaa nje ya dimba kwa miezi tisa.

“Daniel tulimpeleka Afrika Kusini Machi 26 na baada ya uchunguzi ikaonekana kwamba amepata matatizo ya kukatika mtulinga wa kati wa goti na pia ikaonekana vilevile amechanika washa ‘meniscus’ ambayo ipo katikati ya goti na pia vilevile ameonekana ana sehemu ndogo iliyovunjika katika sehemu ya juu ya mfupa wa ugoko ‘tibia’ karibu na maungio ya goti,” alisema.

Alisema amemuacha mchezaji huyo jijini Cape Town, ambapo keshokutwa Jumatano atalazwa katika Hospitali ya Vincent Pallotti kabla ya kesho yake kufanyiwa upasuaji na kukaa hospitali hadi Ijumaa hii.

“Aprili 9 ataonwa na daktari na itakapofika tarehe 10 (kesho yake) atarudi hapa Dar es Salaam, suala na Amoah ni la kusikitisha kidogo kwa sababu ule utaratibu wake baada ya operesheni na kurudia tena kwenye ushindani utamchukua muda wa miezi tisa kwa hiyo ataonekana tena uwanjani baada ya miezi tisa kupita toka siku aliyoumia ambayo ni wiki nane zilizopita kwa hiyo bado miezi mingine saba,” alisema.

Akizungumzia matibabu ya Junior nchini humo, Mwankemwa alisema kuwa mchezaji huyo hajakutwa na tatizo kubwa ambapo atatakiwa kupumzika kwa muda wa siku tano.

“Wazir Junior yeye aliumia kifundo cha mguu na kule alienda aliangaliwa na akapatiwa matibabu ya sindano na pia vilevile akashauriwa kupumzika kwa siku tano, kwa hiyo ataanza mazoezi ya kwenye sehemu za tifutifu (mchanga) siku ya Aprili 5 (Alhamisi) na 6 (Ijumaa) na atajiunga mazoezini na wenzake ambao watakuwa hawajakwenda safari ya Mbeya,” alisema.

Kupata taarifa kamili, ikiwemo ya beki David Mwantika, fungua linki hii: https://youtu.be/k8tRbzouwGw