BEKI wa Azam FC, David Mwantika, anaendelea vizuri baada ya kupata hitilafu ya mwili wakati wa mchezo wa wa robo fainali ya Kombe la Shirikisho (Azam Sporst Federation Cup) dhidi ya Mtibwa Sugar usiku wa kuamkia leo.

Mwantika alipata tatizo hilo dakika ya 64 na kupatiwa matibabu ya awali kabla ya kukimbizwa Hospitali ya Mbagala Zakhem na kuhamishiwa Hospitali ya Wilaya ya Temeke, na baadaye ile ya Rufaa ya Muhimbili (MNH).

Daktari wa Azam FC, Dr. Mwanandi Mwankema, anayeshughulikia taratibu za matibabu yake ameuambia mtandao rasmi wa klabu www.azamfc.co.tz muda mchache uliopita kuwa beki huyo anaendelea vizuri na matibabu katika Hospitali ya Rufaa ya Muhimbili.

“Alikuwa kwenye hali mbaya mara baada ya kumkimbiza hospitali, alikuwa amezimia lakini tunashukuru Mungu kwa sasa anaendelea vizuri, alipata matibabu ya awali Mbagala Zakhem kabla ya kuomba ahamishiwe Muhimbili baada ya kwenda Hospitali ya ya Wilaya ya Temeke zoezi lililokamilika saa saba usiku.

“Tunamshukuru Mungu majira ya saa 10 alfajiri alizinduka na kuanza kuwatambua watu na kuongea, na asubuhi ya leo amekunywa chai vizuri na kuendelea na matibabu huku akiwa yupo kwenye hatua za kuruhusiwa kurejea nyumbani baada ya kupata nafuu,” alisema.

Aidha taratibu zinazofanyika hivi sasa kabla ya kuruhusiwa, ni beki huyo kufanyiwa uchunguzi wa moyo ili kufahamu kuwa kama ana tatizo hilo.

“Mara baada ya kujisikia vizuri kabla ya kuruhusiwa kuondoka hivi sasa amehamishiwa kwenye wodi ya Taasisi ya Jakaya Kikwete inayojihusisha na matatizo ya moyo, ambapo atafanyiwa uchunguzi wa moyo ili kujua kama ana tatizo hilo na baadaye watatoa majibu ya vipimo na ushauri mwingine kwa wanavyomuona,” alimalizia Dr. Mwankemwa.