HAUKUWA usiku mzuri jana kwa Klabu Bingwa ya Afrika Mashariki na Kati, Azam FC, baada ya kutolewa kwenye michuano ya Kombe la Shirikisho (Azam Sports Federation Cup) ikifungwa na Mtibwa Sugar kwa mikwaju ya penalti 9-8 kufuatia dakika 90 kumalizika kwa suluhu.

Mchezo huo uliofanyika Uwanja wa Azam Complex, ulikuwa ni mkali na wa aina yake, ambapo Azam FC itabidi ijilaumu baada ya kupoteza nafasi takribani nne za kufunga mabao dakika 30 za mwanzo za mtanange huo.

Matokeo hayo yanaifanya Azam FC kupoteza nafasi moja ya uwakilishi kwenye michuano ya Afrika mwakani kwani bingwa wa ASFC hukata tiketi ya kushiriki Kombe la Shirikisho Afrika.

Baada ya dakika 90 kumaliza kwa timu zote kwenda suluhu, ilibidi mchezo uamuliwe kwa changamoto ya mikwaju ya penalti, hatua ambayo ilishudiwa Mtibwa Sugar ikiibuka kidedea kwa penalti 9-8, wakikosa mkwaju mmoja na Azam FC ikikosa miwili.

Uhodari wa makipa wote ulionekana usiku huo, kipa Azam FC akicheza mkwaju mmoja uliopigwa na kiungo Henry Joseph huku kipa wa Marcos Tinoko wa Mtibwa naye akipangua mkwaju wa mwisho wa Azam uliopigwa na beki Abdallah Kheri, kabla ya hapo kiungo Frank Domayo ‘Chumvi’, naye alitangulia kukosa akigongesha mwamba.

Aidha penalti nane ilizopata Azam FC, ziliwekwa nyavuni na Nahodha Himid Mao ‘Ninja’, Yahya Zayd, Bruce Kangwa, Agrey Moris, Joseph Kimwaga, Joseph Mahundi, Swaleh Abdallah na Salum Abubakar ‘Sure Boy’.

Mtibwa Sugar waliofunga ni kiungo Hassan Dilunga, Ismail Muhesa, Stamili Mbonde, Shaaban Nditi, Hassan Isihaka, Hassan Mganga, Salim Kihimbwa, Cassian Ponera na beki Dickson Daudi, aliyefunga iliyowapa ushindi.

Ushindi huo unaifanya Mtibwa kukutana na Stand United katika mchezo wa nusu fainali ya michuano hiyo, Stand iliyofuzu hatua hiyo baada ya kuichapa Njombe Mji bao 1-0.

Timu nyingine iliyofuzu hatua ya nusu fainali jana ni JKT Tanzania, ambayo imewafunga wenyeji, Tanzania Prisons mabao 2-0, mchezo uliofanyika Uwanja wa Sokoine mjini Mbeya, ambapo hivi sasa wanamsubiri mshindi wa leo kati ya Singida United na Yanga watakayekutana naye katika hatua hiyo.

Yahya Zayd apewa tuzo yake

Katika mchezo huo pia ilishuhudiwa mshambuliaji wa Azam FC, Yahya Zayd, akikabididhiwa tuzo yake ya Mchezaji Bora wa Azam FC (NMB Player Of The Month) mwezi Februari, tuzo inayotolewa na mdhamini mkuu wa timu hiyo, Benki ya NMB inayoongoza hapa nchini.

NMB wameiongezea ubora zaidi tuzo hiyo, ambapo mwaka huu kwa kuanzia na Zayd wameanza kutoa zawadi ya pesa taslimu Sh. 500,000, ambapo usiku wa jana mchezaji huyo alikabidhiwa hundi ya kiasi hicho cha fedha.

Kikosi cha Azam FC

Mwadini Ally, David Mwantika/Swaleh Abdallah dk 66, Bruce Kangwa, Abdallah Kheri, Agrey Moris, Himid Mao (C), Salum Abubakar, Frank Domayo, Shaaban Idd/Joseph Kimwaga dk 74, Yahya Zayd, Idd Kipagwile/Joseph Mahundi dk 78