ZIMEBAKIA siku nne kabla ya kikosi cha Klabu Bingwa ya Afrika Mashariki na Kati, Azam FC, haikijavaana na Mtibwa Sugar kwenye mchezo wa robo fainali ya Kombe la Shirikisho (Azam Sports Federation Cup) utakaofanyika Uwanja wa Azam Complex Jumamosi hii sa 1.00 usiku.

Wakati kikosi hicho kikienda kucheza na Mtibwa Sugar, leo tunaangalia rekodi za timu zote mbili kwenye mechi sita zilizopita za mashindano yote.

Azam FC inaonekana kuwa moto, baada ya kushinda mechi nne kati ya sita na kutoka sare mbili, ilishinda mfululizo dhidi ya KMC (3-1) ukiwa ni mchezo hatua ya 16 bora ya michuano hiyo, ikazifunga Singida United (1-0), Mwadui (1-0) na Mbao (2-1), lakini katika mechi mbili za awali ilitoka sare ugenini ilipocheza na Kagera Sugar (1-1) na Lipuli (0-0), zote zikiwa za Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara (VPL).

Mtibwa Sugar imeonekana kuwa rekodi mbaya kabisa kwani katika mechi sita zilizopita imeshinda mchezo mmoja tu dhidi ya Buseresere mabao 3-0 kwenye hatua ya 16 bora ya ASFC, huku katika mechi tano za ligi zilizobakia ikifungwa mara nne ilipokipiga na Stand United (2-1), Mtibwa Sugar (3-1), Ruvu Shooting (2-1), Tanzania Prisons (2-1) na kutoka suluhu na Mbao.

Rekodi ASFC

Aidha kabla ya Azam FC kukutana na KMC kwenye hatua iliyopita ya ASFC, katika hatua za awali ilizifungwa Area C United (4-0), Shupavu (5-0) huku Mtibwa Sugar nayo ikizifungashia virago Villa Squad ya Kinondoni kwa mabao 2-1 na kupata ushindi kama huo dhidi ya Maji Maji Rangers ya mkoani Lindi kabla ya kutinga hatua ya 16 bora na kuitoa Buseresere, ambao nni mabingwa wa Mkoa wa Geita.

Kauli ya Kocha Azam FC

Kocha Msaidizi wa Azam FC, Idd Nassor Cheche, amezungumza na mtandao rasmi wa klabu www.azamfc.co.tz kuhusu mchezo huo na kukiri kuwa utakuwa ni mgumu na wa ushindani kutokana na uzuri wa timu zote mbili.

“Mchezo huu ni muhimu sana kwetu mshindi atasogea mbele zaidi kwenye nusu fainali na ukichukua kombe utapata nafasi ya kuwakilisha nchi kwenye michuano ya Kombe la Shirikisho Afrika, na sisi ni nafasi pekee ambayo kwetu sisi tunaiona ni nafasi ya dhahabu kuigombea hii ili kutimiza malengo yetu,” alisema.

Itakumbukwa kuwa msimu huu tayari timu hizo zilikutana kwenye ligi na ikashuhudiwa zikitoka sare ya bao 1-1, bao la Azam FC likitiwa kimiani na winga Enock Atta huku lile la kusawazisha la Mtibwa Sugar likiwekwa nyavuni kwa njia ya mpira wa adhabu ndogo ya moja kwa moja na mshambuliaji Kelvin Sabato ‘Kiduku’.