KIKOSI cha timu ya vijana ya Azam FC chini ya umri wa miaka 20 (Azam U-20) leo kimeipa mazoezi timu Taifa ya Tanzania chini ya umri wa miaka 17 (Serengeti Boys) katika mchezo maalumu wa kirafiki wa mazoezi uliofanyika Uwanja wa Karume, Ilala, Dar es Salaam.

Ilishuhudiwa vijana wa Azam U-20 wakiibuka kidedea kwa ushindi wa bao 1-0, lililofungwa na Hamadi Aziz, dakika ya nane akitumia vema pasi ya Mahamud Said, na kudumu kwa dakika zote 90 za mchezo huo.

Serengeti Boys inayonolewa na Kocha Oscar Milambo, chini ya Mkurugenzi wa Soka la Vijana ndani ya TFF, Kim Poulsen, iliweza kuonyesha upinzani mkali licha ya kufungwa bao hilo jambo ambalo linaonyesha mwanga kuelekea Fainali za Mataifa ya Afrika kwa Vijana wa umri huo zitakazofanyika nchini mwakani.

Mechi hiyo ilikuwa ni maalumu kwa ajili ya kuwapa mechi ya ushindani vijana hao wa Serengeti Boys, ambao wanaendelea na programu kali kuelekea fainali hizo.