KLABU Bingwa ya Afrika Mashariki na Kati, Azam FC, imeichapa Friends Ranger mabao 5-0 katika mchezo wa kirafiki uliomalizika usiku huu kwenye Uwanja wa Azam Complex, Chamazi, Dar es Salaam.

Mchezo huo ulikuwa ni maalum kwa ajili ya wachezaji wa Azam FC kupata mechi ya ushindani kufuatia kusimama kwa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara (VPL) kupisha mechi za kirafiki zilizo katika kalenda ya Shirikisho la Soka la Kimataifa (FIFA).

Vilevile benchi la ufundi la Azam FC limeutumia mchezo huo kama sehemu ya kupasha misuli kuelekea mtanange wa robo fainali ya Kombe la Shirikisho (Azam Sports Federation Cup) dhidi ya Mtibwa Sugar utakaofanyika Uwanja wa Azam Complex Machi 31 mwaka huu saa 1.00 usiku.

Azam FC ilianza vema mchezo huo na kujipatia bao la uongozi dakika ya nne tu, lililofungwa na winga Enock Atta kwa mkwaju wa penalti kufuatia Idd Kipagwile kuangushwa kwenye eneo la hatari.

Uzembe wa safu ya ulinzi ya Friends uliinufaisha tena Azam FC dakika ya 40 baada ya mshambuliaji Mbaraka Yusuph, kuipatia bao la pili na kufanya timu yake iende mapumziko ikiwa na uongozi wa mabao hayo mawili.

Kipindi cha pili ilishuhudiwa winga wa Azam FC, Joseph Kimwaga, akiingia uwanjani dakika ya 67 kuchukua nafasi ya Mbaraka, ikiwa ni mechi yake ya kwanza msimu huu baada ya kupata majeraha ya goti wakati timu hiyo ikijiandaa kucheza mchezo wa kwanza wa ligi dhidi ya Ndanda mkoani Mtwara.

Dakika ya 73 kiungo Salmin Hoza, alitumia jitihada binafsi na kuipatia bao la tatu Azam FC kwa shuti la umbali wa takribani mita 30 lililomshinda kipa wa Friends, Ndugu Juma.

Kimwaga aliyeingia na moto katika kipindi hicho ukiwa ni mchezo wake wa kwanza, alihitimisha ushindi mnono wa Azam FC kwa kufunga mabao mawili dakika ya 75 na 82 huku akishangiliwa na mashabiki waliohudhuria mtanange huo.

Mara baada ya mchezo huo, kikosi cha Azam FC kinatarajia kupumzika kesho Jumapili kabla ya kurejea mazoezini Jumatatu ijayo jioni kumalizia maandalizi ya kuikabili Mtibwa Sugar katika mchezo muhimu kabisa.