MKUU wa Maendeleo ya Soka la Vijana Azam FC, Tom Legg, ameweka wazi mipango aliyojiweka mwaka huu katika timu ya vijana chini ya umri wa miaka 17 (Azam U-17).

Kocha huyo raia wa Uingereza amesema tayari ameanzisha timu ya chini ya umri wa miaka 17, ambayo ameanza kufanya nayo mazoezi tokea mwezi uliopita huku akifurahishwa na vijana wake 10 kuitwa katika kikosi cha timu ya Taifa ya vijana ya Tanzania chini ya umri wa miaka 17 ‘Serengeti Boys’.

Legg anatarajia kuwaona vijana wake 10 hao waliopo timu ya Taifa kesho Jumamosi saa 2.00 asubuhi kwenye mchezo wa kirafiki dhidi ya timu ya vijana ya Azam FC (Azam U-20) utakaofanyika Uwanja wa Karume. 

“Mechi hii itatupa nafasi ya kuwaona wachezaji wetu chini ya umri wa miaka 17 wakichezea timu ya Taifa dhidi ya Azam FC U-20, tunafurahia sana maendeleo kwani bado ni mapema wachezaji wamekuwa pamoja tokea Februari na sasa ni takribani wiki nne tu,” alisema Legg wakati akizungumza na mtandao rasmi wa klabu www.azamfc.co.tz.

Alisema wachezaji alionao kwenye kikosi cha Azam U-17 bado ni wadogo sana huku akidai kuwa amefanya hivyo kutokana na kuwapandisha wachezaji wengi aliokuwa nao mwaka jana katika kikosi cha Azam U-15 walioshiriki Ligi ya Vijana ya Azam (Azam Youth League U-15) na timu yake kushika nafasi ya pili nyuma ya Bom Bom.

“Pia timu ya Taifa nayo inawachezaji wadogo sana wa U-17, hivyo wachezaji wa Serengeti Boys hawana umri wa miaka 17 na 16 bali wana umri miaka 14 na 15, kwa sababu Taifa linajiandaa na michuano ya Mataifa ya Arika ya vijana (AFCON U-17) inayofanyika nchini mwaka 2019,” alisema Legg.

Kushiriki michuano miwili

Moja ya mipango mingine aliyogusia Legg kwa kikosi chake cha U-17, ni kushiriki michuano miwili mwaka huu, akidai kuwa: “Tunatakiwa kuandaa michuano ya vijana ya Azam Dar es Salaam pia tunaweza kusafiri nje ya Dar es Salaam kucheza hapa Tanzania au nje ya Tanzania ili kuwapa vijana fursa ya kucheza soka la ushindani.”

Kuwapeleka vijana nje ya nchi

Legg aliyeanza kibarua chake hicho ndani ya Azam FC miaka miwili iliyopita, alisema katika kukuza vipaji vya wachezaji wake, amepanga kuwapeleka vijana kadhaa wakajifunze kwenye vituo vingine vya kukuza soka nje ya nchi.

“Nitajaribu kuwapa nafasi baadhi ya wachezaji wangu kushiriki mazoezi nje ya Tanzania hivyo moja ya mipango yangu mwaka huu ni sisi kupanga na baadhi ya timu kubwa nje ya Tanzania kuwachukua baadhi ya wachezaji wetu wa kituo chetu mmoja au wawili kwa kipindi kifupi cha muda kwa wiki nne hadi sita kabla ya kurejea nchini,” alisema.

Alisema moja ya malengo ya kufanya ni hivyo ni kuwapa fursa wachezaji wa kikosi hicho kucheza soka nje ya Tanzania kama walivyompeleka Tenerife ya Hispania, Farid Mussa pamoja na kutambua namna wachezaji wa nchi nyingine wanavyoandaliwa.

Kupata mahojiano yote kamili, fungua linki hii: https://youtu.be/HikMgDi_DLQ