TIMU ya vijana ya Azam FC chini ya umri wa miaka 20 (Azam U-20) imeendelea kugawa dozi kama kawaida baada ya kuichapa timu ya jeshi ya Navy kutoka Kigamboni mabao 4-1.

Mchezo huo wa kirafiki uliofanyika Uwanja wa Azam Complex, Chamazi ulikuwa na ushindani mkubwa ambapo kikosi cha Azam U-20, kilijipatia mabao mawili kwenye kila kipindi cha mtanange huo.

Mabao ya Azam U-20 yamefungwa na Hamadi Aziz, aliyefunga la kwanza akimalizia pande safi la Mahamud Said, dakika chache kabla ya mpira huo kwenda mapumziko Mahamud aliongeza bao la pili akitumia vema uzembe wa safu ya ulinzi ya Navy.

Mabadiliko ya Kocha Mkuu wa Azam U-20, Meja Abdul Mingange, ya kuwaingiza kipindi cha pili wachezaji Jamal Abdul na Tepsi Evance, yaliongeza uhai kwenye safu ya ushambuliaji na kujikuta timu hiyo ikijiongezea mabao mengine mawili yote yakifungwa kiufundi na Tepsi.

Azam U-20 imetoa dozi hiyo baada ya wiki iliyopita kuichapa Sweya SC mabao 15-1 katika mchezo mwingine wa kirafiki.