KLABU Bingwa ya Afrika Mashariki na Kati, Azam FC, inatarajia kunoa makali yake kwa kukipiga na Friends Ranger kwenye mchezo wa kirafiki unaotarajia kufanyika Uwanja wa Azam Complex, Chamazi, Dar es Salaam Jumamosi hii saa 1.00 usiku.

Mchezo huo ni maalum kabisa kwa ajili ya kuwaweka wachezaji kwenye ushindani kutokana na kusimama kwa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara (VPL) kupisha mechi za Kimataifa za kirafiki zilizo katika kalenda ya Shirikisho la Soka la Kimataifa (FIFA).

Aidha Azam FC inayoendelea na mazoezi makali kwenye viunga vyake vya Azam Complex, itautumia mchezo huo kama sehemu ya kujiweka sawa kuelekea mchezo wa robo fainali ya Kombe la Shirikisho (Azam Sports Federation Cup) dhidi ya Mtibwa Sugar utakaofanyika uwanjani hapo Machi 31 mwaka huu saa 1.00 usiku.