KLABU Bingwa ya Afrika Mashariki na Kati, Azam FC, kwa sasa ipo kwenye maandalizi ya makali kuelekea mchezo ujao wa hatua ya robo fainali ya Kombe la Shirikisho (Azam Sports Federation Cup) dhidi ya Mtibwa Sugar utakaofanyika Uwanja wa Azam Complex Machi 31 mwaka huu saa 1.00 usiku.

Zimebakia takribani siku 12 kuelekea mchezo huo, ambapo tayari kikosi cha Azam FC kimeanza maandalizi toka Alhamisi iliyopita chini Kocha Mkuu, Aristica Cioaba, ambaye anauchukulia uzito mkubwa mchezo huo na moja ya malengo yake makubwa ni kuiwezesha timu hiyo kutwaa taji hilo na kukata tiketi ya kushiriki Kombe la Shirikisho Afrika mwakani.

Patashika ya Kombe la FA inarejea huku Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara (VPL) ikiwa imeenda mapumziko ya takribani wiki nne, kwa kiasi kikubwa ikiathiriwa na mechi za kirafiki za Kimataifa zilizo katika kalenda ya Shirikisho la Soka la Kimataifa (FIFA).

Wakati ligi hiyo ikienda mapumzikoni, Azam FC imefanikiwa kucheza mechi 22 za ligi ikiwa nafasi ya tatu kwa pointi 44 baada ya ushindi mechi 12, sare nane na kupoteza mechi mbili, ikifunga mabao 24 na kuruhusu nyavu zake kuguswa mara 10.

Mchezaji aanayeongoza kutupia mabao kwenye ligi kwa upande wa Azam FC ni mshambuliaji Yahya Zayd, aliyefunga manne, huku beki wa kushoto Bruce Kangwa, akiwa kinara wa kutoa pasi za mwisho za mabao akifanya hivyo mara tano akifuatiwa na Zayd aliyetoa nne.

Kipa wa Azam FC, Razak Abalora, aliyedaka mechi 19 amefungwa mabao tisa tu huku kwa upande wake Mwadini Ally, aliyedaka mechi tatu zilizopita za Azam FC baada ya Mghana huyo kufungiwa, akiwa ameruhusu bao moja ndani ya dakika 270 (sawa na mechi tatu).