WACHEZAJI watatu wa Klabu Bingwa ya Afrika Mashariki na Kati, Azam FC, Nahodha Himid Mao ‘Ninja’, washambuliaji Shaaban Idd na Yahya Zayd wanatarajia kuripoti kwenye kambi ya timu ya Taifa ya Tanzania ‘Taifa Stars’ leo Jumapili saa 9 alasiri.

Himid na Shaaban wameongezwa Stars na Kocha Mkuu, Salum Mayanga, hivi karibuni baada ya awali kutangulia kumuita Zayd pekee katika kikosi hicho kwa upande wa Azam FC.

Kambi hiyo ya Stars inayoanza leo, inajiandaa na mechi mbili za Kimataifa za kirafiki zilizo katika kalenda ya Shirikisho la Soka la Kimataifa (FIFA) mwezi huu, itaanza kukipiga na Algeria ‘The Green’ Machi 22 jijini Algiers kabla ya kurejea nyumbani, Dar es Salaam kuwakaribisha DR Congo ‘The Leopards’ Machi 27 kwenye Uwanja wa Taifa.

Wachezaji wengine walioitwa, ni pamoja na makipa Aishi Manula, Abdulrahman Mohamed, Ramadhan Kabwili, mabeki ni Shomari Kapombe, Hassan Kessy, Gadiel Michael, Kelvin Yondani, Abdi Banda na Erasto Nyoni.

Viungo ni Hamis Abdallah, Mudathir Yahya, Said Ndemla, Faisal Salum, Abdulaziz Makame, Farid Mussa, Thomas Ulimwengu, Ibrahim Ajibu, Shiza Kichuya, Mohamed Issa, huku washambuliaji wakiwa ni Mbwana Samatta, Saimon Msuva na John Bocco ‘Adebayor’.