ROBO fainali ya Kombe la Shirikisho (Azam Sports Federation Cup) kati ya Klabu Bingwa ya Afrika Mashariki na Kati, Azam FC na Mtibwa Sugar sasa itafanyika Machi 31 mwaka huu kwenye Uwanja wa Azam Complex, Chamazi, Dar es Salam saa 1.00 usiku.

Mchezo huo unasubiriwa kwa hamu na mashabiki wengi wa soka, Azam FC ikiwa imejidhatiti kutinga nusu fainali kwa kuichapa timu hiyo ikiwa ni katika kutimiza malengo ya kulitwaa taji hilo.

Kikosi cha Azam FC kilichokuwa kwenye mapumziko ya siku nne, kinatarajia kuanza rasmi mazoezi kesho Alhamisi tayari kuivutia kasi Mtibwa Sugar.

Mshindi wa mchezo huo, ataenda kucheza ugenini na mshindi wa mechi nyingine ya robo fainali kati ya Stand United na Njombe Mji, watakaocheza Machi 30 kwenye Uwanja wa Kambarage, Shinyanga saa 10.00 jioni.

Mbali na mechi hizo, Machi 31 Tanzania Prisons itawakaribisha JKT Tanzania kwenye Uwanja wa Sokoine, Mbeya mchezo utakaoanza saa 10.00 jioni, huku Aprili Mosi hatua ya robo fainali ikimalizika kwa Singida United kukipiga na Yanga Uwanja wa Namfua, Singida saa 10.00 jioni.

Aidha mbali na bingwa wa michuano hiyo kubeba kombe, medali na kitita cha Sh. milioni 50, pia atakata tiketi ya kuliwakilisha Taifa kwenye michuano ya Kombe la Shirikisho Afrika mwakani.