KLABU Bingwa ya Afrika Mashariki na Kati, Azam FC, imezidi kufanya kweli baada ya kuichapa Mbao mabao 2-1, mchezo uliomalizika usiku huu kwenye Uwanja wa Azam Complex, Chamazi.

Licha ya Simba na Yanga kuwa na mechi mbili mkononi kila mmoja, lakini matokeo hayo yanaifanya Azam FC kusogea hadi nafasi ya pili ikifikisha pointi 44 ikiizidi Yanga pointi moja huku ikizidiwa pointi mbili na Simba iliyo kileleni kwa pointi 46.

Mabao ya Azam FC iliyopata ushindi wa tatu mfululizo, yamefungwa kiustadi na wachezaji waliotokea benchi kipindi cha pili, alianza winga Idd Kipagwile, dakika ya 63 akimalizia kwa kichwa krosi safi ya beki wa kushoto Bruce Kangwa.

Kipagwile alifunga bao hilo la uongozi sekunde chache mara baada ya kuingia kuchukua nafasi ya Joseph Mahundi, na kuamsha kelele kwa mamia ya mashabiki wa Azam FC waliohudhuria mchezo huo.

Dakika tisa baadaye mshambuliaji Bernard Arthur, aliyeingia dakika ya 61 kuchukua nafasi ya Shaaban Idd, aliipatia bao la pili Azam FC kwa jitihada binafsi akimalizia pasi safi ya juu ya kiungo Salum Abubakar ‘Sure Boy’, ambaye amekuwa kwenye kiwango bora kabisa hivi sasa.

Mbao ilijitutumua na kupata bao la kufutia machozi dakika ya 89, lililofungwa na James Msuva, mdogo wake na staa wa Tanzania, Simon Msuva, anayesakata soka la kulipwa nchini Morocco hivi sasa.

Mara baada ya mchezo huo, kikosi cha Azam FC kinatarajia kupumzika kwa siku nne hadi Alhamisi ijayo kitakapoanza tena maandalizi ya kujiandaa na mchezo wa robo fainali ya Kombe la Shirikisho (Azam Sports Federation Cup) dhidi ya Mtibwa Sugar Machi 30 mwaka huu.

Kikosi cha Azam FC:

Mwadini Ally, David Mwantika, Bruce Kangwa, Abdallah Kheri, Agrey Moris, Himid Mao (C), Salum Abubakar, Frank Domayo, Shaaban Idd/Arthur dk 61, Yahya Zayd, Joseph Mahundi/Kipagwile dk 63