MSHAMBULIAJI wa Klabu Bingwa ya Afrika Mashariki na Kati, Yahya Zayd, ameshinda Tuzo ya Mchezaji Bora wa timu hiyo (NMB Player Of The Month) mwezi Januari-Februari.

Zayd ametwaa tuzo hiyo akiwazidi wachezaji wenzake Nahodha Msaidizi Agrey Moris na kiungo Salmin Hoza, baada ya mashabiki kumpigia kura 102 kati ya 144 zilizopigwa sawa na asilimia 70.8 huku Moris akipata 27 (18.8%) na Hoza 15 (10.4%).

Mshambuliaji huyo anakuwa mchezaji watano kutwaa tuzo hiyo tokea ianzishwe msimu huu, ikidhaminiwa na wadhamini wakuu wa Azam FC, Benki ya NMB, wengine waliotangulia wakiwa ni Yakubu Mohammed (Agosti), Mbaraka Yusuph (Septemba-Oktoba), Himid Mao (Oktoba-Novemba), Razak Abalora (Desemba-Januari).

Aidha hiyo ni tuzo ya pili Zayd kuchukua msimu huu, tuzo ya kwanza akichukua kupitia timu ya vijana ya Azam FC (Azam U-20) baada ya kuwa Mchezaji Bora wa timu hiyo (Uhai Player Of The Month) mwezi Desemba-Januari.

Katika hatua nyingine; beki kisiki wa kati wa timu ya vijana ya Azam FC aliyepandishwa kikosi cha wakubwa, Oscar Masai, amefanikiwa kuwa mchezaji bora kwa upande wa timu ya vijana (Uhai Player Of The Month) Januari-Februari baada ya kuwa na mchango mkubwa kwenye timu hiyo.

Wengine waliotwaa tuzo hiyo inayodhaminiwa na wadhamini namba mbili wa Azam FC, maji safi ya Uhai Drinking water, kwa upande wa Azam B kabla ya Masai ni pamoja na kiungo Twaha Rajab (Agosti) na washambuliaji Paul Peter (Septemba-Oktoba), Andrew Simchimba (Oktoba-Novemba), Yahya Zayd (Desemba-Januari).

Tuzo za washindi wote zinatarajia kutolewa kesho Jumapili kabla ya mchezo wa Azam FC dhidi ya Mbao, utakaofanyika Uwanja wa Azam Complex, Chamazi, Dar es Salaam saa 1.00 usiku.