MSHAMBULIAJI wa Klabu Bingwa ya Afrika Mashariki na Kati Azam FC, Yahya Zayd, ni miongoni mwa nyota 23 walioitwa kwenye kikosi kipya cha timu ya Taifa ya Tanzania ‘Taifa Stars’ kinachojiandaa na mechi mbili za kirafiki dhidi ya Algeria na DR Congo.

Stars inatarajia kucheza mechi mbili za kirafiki zilizo katika kalenda ya Shirikisho la Soka la Kimataifa (FIFA) mwezi huu, ikianzia ugenini jijini Algiers kuivaa Algeria ‘The Greens’ Machi 22 kabla ya kurejea nyumbani, Dar es Salaam kuwakaribisha DR Congo ‘The Leopards’ Machi 27 kwenye Uwanja wa Taifa.

Wachezaji wengine walioitwa na Kocha Mkuu wa timu hiyo, Salum Mayanga leo, ni pamoja na makipa Aishi Manula, Abdulrahman Mohamed, Ramadhan Kabwili, mabeki ni Shomari Kapombe, Hassan Kessy, Gadiel Michael, Kelvin Yondani, Abdi Banda na Erasto Nyoni.

Viungo ni Hamis Abdallah, Mudathir Yahya, Said Ndemla, Faisal Salum, Abdulaziz Makame, Farid Mussa, Thomas Ulimwengu, Ibrahim Ajibu, Shiza Kichuya, Mohamed Issa, huku washambuliaji wakiwa ni Mbwana Samatta, Saimon Msuva na John Bocco, wanaoungana na Zayd.