IKIWA katika morali nzuri kabisa, Klabu Bingwa ya Afrika Mashariki na Kati Azam FC, itakuwa kwenye vita kali ya kuhakikisha inavuna pointi tatu muhimu pale itakapokuwa ikikabiliana na Mwadui kesho Alhamisi saa 1.00 usiku.

Azam FC itakayokuwa kwenye dimba lake la Azam Complex, imetoka kushinda bao 1-0 dhidi ya timu ngumu ya Singida United katika mchezo uliopita wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara (VPL) ulifanyika uwanjani hapo huku Mwadui ikitoka kutoka suluhu na Mbeya City ugenini.

Kuelekea mchezo huo kikosi cha Azam FC kipo vizuri na wachezaji wamekuwa wakionyesha ari kubwa na jitihada kwenye mazoezi hii ikiashiria ni kwa namna gani wamejipanga kupata ushindi katika mchezo huo na mechi nyingine zijazo.

Kocha Msaidizi wa Azam FC, Idd Cheche, tayari amesema kwa sasa hawataruhusu kupoteza mchezo wowote na wamejipanga kupata matokeo mazuri katika mechi zote zilizobakia ikiwemo ya kesho dhidi ya Mwadui.

Azam FC itaendelea kuwakosa nyota wake wanne beki Daniel Amoah, Wazir Junior, Joseph Kimwaga wanaoendelea na programu za mwisho za kurejea dimbani huku beki Yakubu Mohammed, akiwa bado hajaanza mazoezi akiwa anasumbuliwa na majeraha ya mguu.

Pia itaendelea kumkosa kwa mechi ya pili, kipa wake Razak Abalora, aliyefungiwa mechi tatu na Kamati ya Nidhamu ya TFF akidaiwa kumtolea lugha chafu mwamuzi Jonesia Rukyaa, mara baada ya mchezo dhidi ya Simba Februari 7 mwaka huu, anatarajia kumalizia adhabu yake Jumapili hii wakati Azam FC itakapokipiga na Mbao katika mechi ya ligi itakayofanyika Uwanja wa Azam Complex saa 1.00 usiku.

Lakini ubora aliouonyesha kipa namba mbili Mwadini Ally, kwenye mchezo uliopita dhidi ya Singida United unaipa urahisi benchi la ufundi la Azam FC kuweza kuendelea kumwamini kipa huyo ambaye amekuwa sehemu ya mafanikio ya kikosi cha Azam FC kwa miaka yote tokea asajiliwe miaka takribani nane iliyopita.

Ushindi wowote kwa Azam FC dhidi ya Mwadui utaifanya kurejea nafasi ya pili kwenye ligi ikifikisha pointi 41 na kuishusha Yanga itakayokuwa nazo 40 lakini itakuwa na mechi mbili mkononi huku Simba ikiwa kileleni kwa pointi 46.

Hadi sasa, mabingwa hao wa ligi msimu wa 2013/2014 wanaodhaminiwa na Benki ya NMB, Maji safi ya Uhai Drinking Water na Tradegents, wamecheza mechi 20 za ligi ikiwa imeshinda mara 10, sare nane na kupoteza mbili huku ikiwa imefunga jumla ya mabao 21.

Aidha Azam FC ndio timu pekee mpaka sasa iliyoonekana kuwa na ubora mkubwa kwenye eneo la ulinzi baada ya kufungwa mabao machache kwenye ligi hiyo ikiwa imetikiswa nyavu zake mara tisa, huku ikiziacha Simba na Yanga ambazo zimeruhusu nyavu zake kufungwa mara 10 (Yanga) na 11 (Simba).

Kihistoria timu hizo zimekutana mara tano kwenye ligi, mchezo wa kesho ukiwa ni sita ambapo Azam FC imeshinda mara tano na mechi moja ikiisha kwa sare iliyofanyika Uwanja wa Mwadui Complex, matokeo yakiwa 1-1.

Katika mechi zote hizo tano, jumla ya mabao 11 yamefungwa, Azam FC ikizitisa nyavu za Mwadui mara tisa sawa na zaidi ya robo tatu ya mabao yote huku Mwadui ikifunga mabao mawili tu yote yakifungwa Mwadui Complex na winga Hassan Kabunda.