NYOTA watatu wa Klabu Bingwa ya Afrika Mashariki na Kati Azam FC, Nahodha Msaidizi Agrey Moris, kiungo Salmin Hoza na mshambuliaji Yahya Zayd, wamechaguliwa kuwania Tuzo ya Mchezaji Bora wa timu hiyo (NMB Player Of The Month) mwezi Januari-Februari.

Wachezaji hao wamechaguliwa na benchi la ufundi kutokana na viwango vyao bora kwenye miezi hiyo miwili, ambapo inaanzia katika mechi na Majimaji mara baada ya kikosi cha Azam FC kurejea kutoka kushinda taji la Mapinduzi Cup hadi ile ya Kombe la Shirikisho (Azam Sports Federation Cup) dhidi ya KMC zikiwa ni idadi ya mechi 10.

Katika mechi hizo 10, Moris amecheza mechi nane kwa kiwango bora akiingoza vema safu ya ulinzi, Hoza naye akicheza vizuri kwenye eneo la kati la uwanja huku Zayd akifunga jumla ya mabao manne na kutoa pasi nne zilizozaa mabao ikiwa ni rekodi bora kabisa katika eneo la ushambuliaji.

Zoezi hili la mashabiki kupiga kura kumchagua mchezaji bora, linatarajia kuanza rasmi leo hadi Jumamosi saa 6.00 mchana, mshindi atakapotangazwa na kukabidhiwa tuzo yake wakati Azam FC ikicheza na Mbao Jumapili hii kwenye Uwanja wa Azam Complex saa 1.00 usiku.

Hadi sasa tokeo tuzo hiyo ianzishwe msimu huu ikidhaminiwa na wadhamini wakuu wa Azam FC, Benki ya NMB, imeshachukuliwa na wachezaji wanne Yakubu Mohammed (Agosti), Mbaraka Yusuph (Septemba-Oktoba), Himid Mao ‘Ninja’ (Oktoba-Novemba), Razak Abalora (Desemba-Januari).

 

Kuanza kupiga kura yako, BOFYA HAPA: https://poll.fbapp.io/nmb-player-of-the-month-january-february