BAADA ya kuonyesha uwezo mkubwa kwenye mchezo dhidi ya Singida United, Kocha Msaidizi wa Azam FC, Idd Nassor Cheche, ameweka wazi kuwa hali ya kutokata tamaa mazoezini na uzoefu ndivyo vilivyomng’arisha kipa Mwadini Ally kwenye mtanange huo.

Mwadini aliyeingia kwenye kikosi cha kwanza cha Azam FC kwa mara ya kwanza katika mchezo wa Ligi Kuu msimu huu dhidi ya Singida baada ya Razak Abalora kusimamishwa na Bodi ya Ligi, alifanikiwa kuonyesha kiwango bora kabisa akiokoa michomo mingi ya wachezaji wa Singida hasa kipindi cha pili.

Akizungumza mara baada ya mchezo huo na mtandao rasmi wa klabu www.azamfc.co.tz Cheche alisema kipa huyo ni moja ya makipa wazoefu na kufikichua amekuwa akifanya vema kwenye mazoezi ya kila siku ya timu hiyo.

“Mchezaji unamwangalia kwenye mazoezi wachezaji wetu wengi wa kiswahili (Kitanzania) wanapokuwa hawachezi mechi ya kwanza na ya pili na ya tatu anakuwa hafanyi jitihada kwenye mazoezi lakini Mwadini (Ally) toka tumeanza msimu katika mazoezi yuko vizuri n ahata mtu akija anaweza kujiuliza kwa nini hapati nafasi ya kucheza.

“Kwa sababu nafasi ya golikipa akishaanza mmoja anapofanya vizuri sio rahisi kumbadilisha lakini katika mazoezi amekuwa akifanya vizuri zaidi kila siku anapofanya kiasi kwamba ikitokea kitu ukimweka unakuwa huna wasiwasi,” alisema.

Aidha mbali na Mwadini kucheza mechi moja ya ligi, pia msimu huu amecheza mechi moja ya Kombe la Shirikisho (Azam Sports Federation Cup) dhidi ya Shupavu, ambayo Azam FC haikuruhusu nyavu zake kuguswa kwenye ushindi wa 5-0, mabao matatu ‘hat-trick’ yakifungwa na Paul Peter huku mengine yakitupiwa na Yahya Zayd na Idd Kipagwile.

Akizungumzia kiufundi mchezo huo, Cheche alisema ulikuwa ni mchezo mgumu na hawakupata matokeo kirahisi kutokana na upinzani mkali waliounyesha Singida United kadiri dakika zilivyiokuwa zikienda baada ya kupata bao la uongozi.

“Tulivyoanza tuliona kama tunaweza kupata ushindi wa mabao mengi lakini muda ulivyokuwa unakwenda mchezo ulikuwa unazidi kuwa mgumu ulikuwa hautabiriki unakaa kwenye kiti presha ilikuwa juu lakini mwisho wa siku Mungu amejalia tumeweza kupata matokeo tunamshukuru Mungu,” alisema.

Mara baada ya mchezo huo kikosi cha Azam FC kitarejea mazoezini kesho Jumatatu jioni kuanza maandalizi ya mechi mbili zijazo ndani ya wiki moja dhidi ya Mwadui Alhamisi ijayo na Mbao Jumapili ijayo, zote zikipigwa kwenye Uwanja wa Azam Complex, Chamazi, Dar es Salaam.

Wakati huo huo, taarifa zilizoifikia Azam FC kutoka Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) zinaeleza kuwa shauri ya kipa wa timu hiyo, Razak Abalora, la kumtolea lugha chafu mwamuzi Jonesia Rukyaa, kwenye mechi na Simba Februari 7 mwaka huu linatarajia kusikilizwa kesho Jumatatu na Kamati ya Nidhamu.

Abalora ataongozana na Ofisa Mtendaji Mkuu wa Azam FC, Abdul Mohamed, kwenda kusikiliza kesi yake ikiwemo kutoa utetezi wake kabla ya Kamati hiyo kuona kuwa kama anastahili adhabu au la kwa mujibu wa kanuni zinazosimamia mchezo huo wa soka.