KLABU Bingwa ya Afrika Mashariki na Kati, Azam FC, muda mchache uliopita imepangwa kucheza na Mtibwa Sugar katika mchezo wa hatua ya robo fainali ya michuano ya Kombe la Shirikisho (Azam Sports Federation Cup) uliopangwa kufanyika Uwanja wa Azam Complex kati ya Machi 30 na Aprili Mosi mwaka huu.

Droo hiyo ya michuano hiyo, imepangwa kwenye ofisi za wadhamini wakuu, Kampuni ya Azam Media kwa kushirikiana na Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) na kurushwa moja kwa moja kupitia Azam TV, ambapo siku chache zijazo watapanga ratiba rasmi ya tarehe ya mechi zote nne zilizopangwa.

Mechi nyingine tatu zilizobakia, Singida United itaialika Yanga kwenye Uwanja wa Namfua, Singida, Tanzania Prisons itakuwa nyumbani katika Uwanja wa Sokoine, Mbeya kuikaribisha JKT Tanzania huku Stand United inayotumia Uwanja wa Kambarage, mjini Shinyanga ikiikaribisha Njombe Mji.

Azam FC inayodhaminiwa na Benki ya NMB, Maji safi ya Uhai Drinking Water na Tradegents, ikifanikiwa kuitoa Mtibwa, droo hiyo inaonyesha kuwa itacheza na mshindi wa mchezo kati ya Stand na Njombe, safari hii mtanange huo utapigwa ugenini na ikifuzu hapo itaingia moja kwa moja fainali.

Aidha mshindi wa mechi kati ya Singida United na Yanga anatarajia kupambana na mshindi wa robo fainali nyingine kati ya Tanzania Prisons na JKT Tanzania.

Wakati Azam FC ilifuzu hatua hiyo kwa kuichapa KMC mabao 3-1 kwa mabao safi ya Frank Domayo, Yahya Zayd na Mbaraka Yusuph, Mtibwa yenyewe iliwatoa Buseresere kwa ushindi wa 2-0, mchezo uliofanyika Uwanja wa Nyamagana, jijini Mwanza.

Bingwa wa michuano hiyo, anatarajia kuvuna kitita cha Sh. Milioni 50 pamoja na kombe la ubingwa na medali, vilevile atakata tiketi ya kuliwakilisha Taifa kwenye Kombe la Shirikisho Afrika mwakani.