BAADA ya Klabu Bingwa ya Afrika Mashariki na Kati, Azam FC, kushindwa kupata matokeo ya ushindi kwenye mechi tatu zilizopita, beki kisiki wa kushoto wa timu hiyo, Bruce Kangwa, amewahakikishia mashabiki kuwa wataanza na matokeo ya ushindi kuanzia kesho Jumamosi kwa kuichapa KMC.

Mchezo huo wa raundi ya 16 bora ya Kombe la Shirikisho (Azam Sports Federation Cup) utafanyika kwenye Uwanja wa Azam Complex saa 1.00 usiku, ambapo Azam FC itakuwa ikisaka nafasi muhimu ya kutinga hatua ya robo fainali ya michuano hiyo.

Azam FC katika mechi tatu zilizopita za ligi imetoka sare mbili dhidi ya Kagera Sugar (1-1) na Lipuli (0-0), kabla ya hapo ilitoka kupoteza dhidi ya Simba bao 1-0, lakini timu hiyo bado ipo katika vita ya kuwania ubingwa wa ligi hiyo ikiwa na pointi 35 kwenye msimamo, ikizidiwa pointi mbili na Yanga iliyonafasi ya pili na Simba ipo kileleni ikiwa nazo 42, huku timu hizo mbili za juu kila mmoja akiwa na mchezo mmoja mkononi.

Akizungumza na mtandao rasmi wa klabu www.azamfc.co.tz Kangwa aliwaomba mashabiki wajitokeze kwa wingi huku akiahidi kwa niaba ya wachezaji wenzake kuwa wamewaandalia mambo mazuri ikiwemo kuibuka na ushindi katika mchezo huo.

“Ninachoweza kusema nashukuru sana kwa sapoti yenu na asante kwa kila kitu tunathamini sana kila kitu mnachofanya kwa ajili yetu. Tunafanya kazi kwa bidii kwa ajili ya mechi ya Jumamosi (kesho) kila mtu anaangalia mbele na kupambana kushinda mechi hiyo ya Jumamosi,” alisema.

Beki huyo raia wa Zimbabwe anayesifika kwa kasi yake kubwa ya kupandisha mashambulizi na kuisumbua safu ya ulinzi ya wapinzani, alisema morali kwa wachezaji wote iko juu na kila mmoja akifanya kazi vizuri kuhakikisha wanaondoa matokeo mabaya waliyopata kwenye mechi tatu zilizopita za ligi.

“Kocha na benchi la ufundi wamekuwa wakimhamasisha kila mmoja na kila mmoja amekuwa akijihamasisha kushinda mchezo huu kwa sababu mechi tatu zilizopita hatujashinda hata moja, tumepoteza mechi moja na sare mbili, tutaanza na mechi hii ya Jumamosi kushinda,” alisema.

Tayari Kocha Mkuu, Aristica Cioaba, ameshaweka wazi kuwa kikosi chake kinauchukulia kwa uzito mchezo huo na hawataki kufanya makosa yoyote dhidi ya wapinzani wao hao huku akiwataka wachezaji wake kumheshimu mpinzani wanayecheza naye.

“Wachezaji wanafahamu michuano hii kuwa ni migumu kama huweki umakini wa kushinda mchezo basi utapata tatizo kwa kuwa ni mchezo mmoja tu na sio kama ligi, nataka kila mmoja afahamu hali hii na kuonyesha umakini kwenye mchezo huu.

“Nawajua wapinzani wetu kuwa ni timu nzuri, wachezaji wanatakiwa kumuheshimu mpinzani na kuingia Jumamosi uwanjani na kucheza kwa nguvu na kushinda mchezo,” alisema Cioaba alipozungumza na mtandao huu mapema wiki hii.

Hii ni mara ya pili timu hizo zinacheza msimu huu, mara ya kwanza ilikuwa ni kwenye mchezo maalum wa kujiandaa na msimu (pre season), Azam FC ikishinda kwa bao 1-0 lililofungwa kwa mkwaju wa penalti na Nahodha Msaidizi na beki kisiki wa kati aliyecheza kwa mafanikio muda mrefu, Agrey Moris.

Mabingwa hao mara nne wa Kombe la Mapinduzi, wamefika hatua hiyo baada ya kuichapa Shupavu ya Morogoro mabao 5-0, yaliyofungwa na mshambuliaji Paul Peter aliyepiga ‘hat-trick’ huku Idd Kipagwile na Yahya Zayd, nao wakitupia, KMC yenyewe iliichapa Toto Africans 7-0.

Rekodi nzuri FA Cup  

Azam FC kihistoria mpaka sasa imeshacheza mara mbili michauno hiyo tokea irudishwe tena mwaka 2015, na mara zote kikifika hatua za mbali, msimu wa 2015/2016 kikifika fainali na kupoteza kwa kufungwa ya Yanga mabao 3-1 huku msimu uliopita kikiishia nusu fainali baada ya kupoteza kwa bao 1-0 dhidi ya Simba.

Msimu wa 2015/2016 wakati kikifika fainali na kufungwa na Yanga, Azam FC ilikutana na Panone ya mjini Moshi kwenye hatua ya 16 bora katika mechi ngumu iliyofanyika Uwanja wa Ushirika, ambapo matajiri hao walitoka nyuma na kushinda mabao 2-1, yaliyofungwa na nyota wa zamani wa timu hiyo, beki Pascal Wawa na mshambuliaji Allan Wanga.

Aidha msimu uliopita kwenye hatua ya 16 bora iliitoa Mtibwa Sugar kwa kuipa kipigo cha 1-0, mchezo uliofanyika Uwanja wa Azam Complex, Chamazi, Dar es Salaam, bao likifungwa na winga Ramadhan Singano ‘Messi’ aliyepokea pande safi kutoka kwa kiungo machachari Salum Abubakar ‘Sure Boy’.

Safari hii msimu huu, mabingwa hao wa Ligi Kuu msimu 2013/2014 wanaodhaminiwa na Benki ya NMB, Maji Safi ya Uhai Drinking Water na Tradegents, wamefika tena hatua hiyo ya 16 bora na watacheza dhidi ya KMC iliyopanda daraja, Azam FC ikiwa na kila sababu ya kusonga mbele kutimiza lengo la kutwaa taji hilo na kurejea kwenye michuano ya Afrika.

Mbali na bingwa wa michuano hiyo kutwaa Kombe, medali na pesa taslimu Sh. Milioni 50, pia atakata tiketi ya moja kwa moja kushiriki Kombe la Shirikisho Afrika mwaka 2019.