WAKATI nahodha wa Azam FC, Himid Mao ‘Ninja’, akitarajia kukaa nje ya dimba kwa wiki tatu zaidi, habari njema ni kuwa mshambuliaji Wazir Junior, ataanza rasmi mazoezi Jumatatu ijayo.

Wawili hao wanasumbuliwa na majeraha tofauti, Himid akisumbuliwa na maumivu ya chini ya goti la mguu wa kulia huku Junior akikabiliwa na tatizo la kifundo cha mguu (enka), ambayo tayari ameshapatiwa matibabu katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili (MNH) kitengo cha MOI.

Himid ambaye pia Nahodha wa kikosi cha timu ya Taifa ya Tanzania cha Wachezaji wa Ndani (CHAN) na Nahodha Msaidizi wa Taifa Stars, alikwenda kufanyiwa uchunguzi jijini Cape Town, Afrika Kusini katika Hopitali ya Vincent Pallotti, baada ya kupatiwa matibabu ya awali Muhimbili.

Daktari wa Azam FC, Dr. Mwanandi Mwankemwa, mapema leo ameuambia mtandao rasmi wa klabu www.azamfc.co.tz kuwa ripoti ya Dr. Nickolas kutoka Afrika Kusini inamtaka kiungo huyo mkabaji kupumzika kwa takribani wiki sita ili kutibu tatizo linalomkabili.

“Tarehe 16 Februari Himid alifanyiwa kipimo cha MRI na kuonekana kuwa goti lake halina tatizo kitu kilichoonekana tu ni kwamba alikuwa na kama uwekundu au uvimbe (inflammation) katika maungio yake ya mfupa wa ugoko pamoja na sehemu ya juu ya goti ambayo kwa kitaalamu tunaita ‘patellar’.

“Kwa hiyo Himid ameshauriwa apumzike kwa muda wa wiki sita, sasa ukiangalia alishapumzika wiki tatu kwa hiyo kuanzia sasa Himid atapumzika kwa wiki tatu na kurudi tena uwanjani kama kawaida,” alisema daktari huyo mkongwe aliyedumu kwa muda mrefu kwenye tiba za wachezaji.

Akizungumzia maendeleo ya matibabu ya Junior, alisema kuwa tayari hali yake imeanza kuwa vizuri baada ya kupata matibabu MOI na sasa anatarajia kuanza rasmi mazoezi na wachezaji wenzake Jumatatu ijayo.

Naye beki Daniel Amoah, muda wowote kuanzia sasa anatarajia kufanyiwa kipimo cha MRI kuangalia undani wa tatizo lake la goti analolalamika linamsumbua.

Amoah alipata maumivu hayo takribani wiki tano zilizopita wakati Azam FC ikipambana na Stand United, ambapo alianguka pembezoni mwa uwanja kwenye safu ya vigae (pavement) na kudondokea goti kabla ya kupata matibabu na baadaye kurejea uwanjani katika mchezo dhidi ya Simba alipojitonesha tena.

Daktari huyo alimalizia kwa kueleza kuwa, wachezaji wengine wa Azam FC waliobakia wapo vizuri kuelekea mchezo ujao wa Kombe la Shirikisho (Azam Sports Federation Cup) dhidi ya KMC uatakofanyika Uwanja wa Azam Complex Jumamosi hii saa 1.00 usiku.