KLABU Bingwa ya Afrika Mashariki na Kati, Azam FC, imetoka suluhu dhidi ya Lipuli katika mchezo wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara (VPL) uliofanyika Uwanja wa Samora, Iringa jioni ya leo.

Kwa matokeo hayo Azam FC inaendelea kusalia nafasi ya tatu kwenye msimamo wa ligi ikifikisha pointi 35, ikizidiwa pointi mbili na Yanga (37) iliyonafasi ya pili huku Simba ikiwa kileleni kwa pointi 42, zote hizo mbili za juu zikiwa na mchezo mmoja mkononi.

Hiyo ni mechi ya tatu mfululizo Azam FC inashindwa kuibuka na ushindi, mechi zote zikiwa ni za ugenini kufuatia kufungwa bao 1-0 na Simba, sare ya bao 1-1 dhidi ya Kagera Sugar pamoja na suluhu ya leo walipocheza na Lipuli.

Azam FC iliingia kwenye mchezo huo, ikinufaika na urejeo wa Nahodha wake Msaidizi, Agrey Moris, aliyekuwa akitumikia adhabu ya kukosa mechi moja kufuatia kukusanya kadi za njano, winga Joseph Mahundi na mshambuliaji Yahya Zayd, ambao walikuwa wagonjwa.

Aidha Kocha Mkuu, Aristica Cioaba, naye alirejea kukaa benchi baada ya kumaliza adhabu ya kutokalia benchi hilo kwa mechi tatu, aliyopewa na Bodi ya Ligi Kuu Tanzania Bara (TPLB) wakidai alionyesha ishara mbaya kwa mashabiki wakati wa mchezo wa Azam FC dhidi ya Yanga Januari 27 mwaka huu.

Mabingwa hao wa ligi msimu wa 2013/2014 waliuanza vema mchezo huo kwa kasi na dakika ya kwanza tu, winga Idd Kipagwile, aliingia vema kwenye eneo la 18 lakini shuti alilopiga lilitoka pembeni ya lango.

Baada ya shambulizi hilo kwa muda mrefu mpira huo ulikuwa nguvu sawa kwa timu zote kushambuliana kwa zamu, lakini Azam FC ilionekana kukosa maarifa ya namna ya kuipenya safu ya ulinzi ya Lipuli.

Dakika ya 44 Azam FC iliweza kutikisa nyavu za Lipuli baada ya Shaaban Idd kupokea pande zuri kutoka kwa Joseph Mahundi na kuweka mpira kimiani kabla ya mwamuzi msaidizi namna mbili kunyoosha kibendera juu akiashiria mfungaji alikuwa ameotea.

Mabadiliko ya kuingia mshambuliaji Bernard Arthur na kutoka Shaaban, yaliongeza uhai kwenye safu ya ushambuliaji ya Azam FC, ambapo kama mshambuliaji huyo angekuwa makini dakika ya 62 angeifungia bao la uongozi Azam FC baada ya kubakia na kipa lakini shuti alilopiga lilimlenga kipa aliyeupangua mpira na kuokolewa na mabeki.

Hadi zinamalizika dakika 90 matokeo yalibakia hivyo kwa timu zote mbili kugawana pointi moja kila mmoja. Azam FC itaanza safari ya kurejea Dar es Salaam kesho alfajiri tayari kuanza maandalizi ya mchezo ujao wa Kombe la FA (Azam Sports Fedaration Cup) dhidi ya KMC utakaofanyika Uwanja wa Azam Complex Februari 24 mwaka huu saa 1.00 usiku.

Kikosi cha Azam FC leo

Razak Abalora, Swaleh Abdallah, Bruce Kangwa, Yakubu Mohammed, Agrey Moris (C), Stephan Kingue, Joseph Mahundi, Salmin Hoza, Yahya Zayd/Mbaraka Yusuph dk 84, Shaaban Idd/Bernard Arthur dk 46, Idd Kipagwile/Enock Atta dk 63