KLABU Bingwa ya Afrika Mashariki na Kati, Azam FC, itakuwa na kazi moja tu kesho Ijumaa kusaka pointi tatu muhimu ugenini pale itakapokuwa ikimenyana na Lipuli katika mchezo wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara (VPL) utakaopigwa Uwanja wa Samora, mjini Iringa.

Huo utakuwa mchezo muhimu kwa kikosi hicho katika kukirudisha katika mwenendo wa ushindi baada ya kutofanya hivyo kwenye mechi mbili zilizopita kufuatia kufungwa bao 1-0 na Simba na sare ya bao 1-1 dhidi ya Kagera Sugar, zote ikicheza ugenini.

Mabingwa hao wa ligi msimu wa 2013/2014 wataingia uwanjani wakiwa na urejeo wa wachezaji wawili waliokosekana katika mchezo uliopita, ambao ni nahodha msaidizi Agrey Moris, aliyekuwa akitumikiwa adhabu ya kukosa mechi moja kufuatia kukusanya kadi tatu za njano na mshambuliaji Yahya Zayd, aliyeugua homa ghafla wakati timu hiyo ikielekea kucheza na Kagera Sugar.

Lakini itaendelea kuwakosa nyota wake kadhaa, Nahodha Himid Mao ‘Ninja’, aliyekwenda Afrika Kusini kwa matibabu ya goti lake la mguu wa kulia, beki Daniel Amaoh, anayeugusa majeraha kama hayo, mshambuliaji Wazir Junior, anayetarajia kufanyiwa upasuaji mdogo wa kifundo cha mguu na kiungo Salum Abubakar ‘Sure Boy’.

Akizungumza na mtandao rasmi wa klabu www.azamfc.co.tz mchezo huo, Kocha Mkuu wa Azam FC, Aristica Cioaba, alisema kikosi chake kipo kamili tayari kupambana na kuibuka na pointi zote tatu.

“Lakini kwa mechi ya kesho wachezaji wote watakuwepo, Moris atacheza, Yayha Zayd atacheza, nina kikosi kamili isipokuwa kwa Sure Boy ambaye ana matatizo ya familia na ameshindwa kusafiri, amebaki Chamazi kwa programu maalumu, lakini waliobakia wote wapo kamili na wapo tayari kubeba pointi tatu,” alisema.

Cioaba aliongeza kuwa: “Ndio kama mnavyoona tumetoka kucheza na Kagera, hatukucheza vizuri dakika 45 za kwanza sijui ni nini ila baada ya mechi ya Simba morali kwa wachezaji ilishuka, pia baadhi ya wachezaji hawakucheza mfano Moris alikuwa na kadi tatu za njano pia baadhi walikuwa majeruhi, Yahya majeruhi, Daniel majeruhi, Sure alikuwa na matatizo ya kifamilia.

“Tatizo likaja kwenye mabadiliko ya kikosi walicheza wachezaji ambao hawakucheza muda mrefu, lakini baada ya kuzoea mazingira kipindi cha kwanza wakabadilika na kucheza vizuri kipindi cha pili.”

Kocha huyo wa zamani wa Aduana Stars, aliwaomba mashabiki kujitokeza kwa wingi kuisapoti timu, huku akidai kuwa: “Ligi bado mbichi na tuna mashindano mengine pia ya Kombe la Shirikisho (Azam Sports Federation Cup) labda tunaweza kupata nafasi ya kucheza Kombe la Shirikisho Afrika lakini mpira si mchezo wa maneno tunahitaji tupigane uwanjani.”

Naye kiungo Salmin Hoza, alizungumza kwa niaba ya wachezaji wenzake kuelekea mchezo huo na kudai kuwa wana morali kubwa ya kuhakikisha wanapigana na kuibuka na ushindi kesho.

“Tumefanya mazoezi ya mwisho tumejiandaa vizuri tunasubiri siku ya mchezo ifike tuweze kupambana na tuweze kurudi na pointi tatu Dar es Salaam,” alisema.

Alisema timu hiyo kushindwa kupata ushindi katika mechi mbili zilizopita ni hali ya mchezo na kueleza kuwa: “Kuna kipindi mnakuwa vizuri mnapata matokeo lakini kuna wakati matokeo yanakuwa magumu lakini kwa maandalizi tuliyoyafanya tumejiandaa vizuri kuhakikisha kesho tunapata pointi tatu ili tuweze kusonga mbele kwenye msimamo wa ligi kuu.”

Huo utakuwa ni mchezo wa tatu kwa timu hizo kukutana msimu huu, mechi moja ikiwa ni ya maandalizi ya msimu ambayo Azam FC ilishinda 4-0 mjini Iringa, mabao yaliyofungwa na beki Yakubu Mohammed, Zayd, Junior, Sure Boy huku ile ya pili ikiwa ni raundi ya kwanza ya ligi iliyopigwa Uwanja wa Azam Complex, na wenyeji hao kushinda 1-0 kwa bao lililofungwa na mshmbuliaji Mbaraka Yusuph. aliyepokea pasi safi ya Himid.

Hadi sasa ikiwa inaelekea raundi ya 19 ya mechi za ligi, Azam FC inashika nafasi ya tatu kwa pointi 34, ikizidiwa pointi tatu na Yanga (37) iliyonafasi ya pili huku Simba ikiwa kileleni kwa pointi 42 baada ya sare ya mabao 2-2 waliyoipata leo dhidi ya Mwadui.