NAHODHA wa Klabu Bingwa ya Afrika Mashariki na Kati Azam FC, Himid Mao ‘Ninja’, anatarajiwa kuelekea jijini Cape Town, nchini Afrika Kusini kesho Alhamisi kufanyiwa uchunguzi wa goti la mguu wake kulia linalomsumbua.
Ninja ambaye amekosa takribani mechi nne zilizopita za Azam FC baada ya kupewa mapumziko maalum kupisha matibabu ya tatizo hilo, amekuwa nguzo muhimu ya timu hiyo na timu ya Taifa ya Tanzania ‘Taifa Stars’ katika eneo la kiungo cha ukabaji na baadhi ya mechi akitumika kama beki wa kulia.
Daktari Mkuu wa Azam FC, Dr. Mwanandi Mwankemwa, ameuambia mtandao rasmi wa klabu www.azamfc.co.tz kuwa Nahodha huyo Msaidizi wa Stars atafanyiwa uchunguzi huo katika Hospitali ya Vincent Pallotti mjini humo ili kujua undani wa tatizo lake huku akidai ataanza kuchukuliwa vipimo na Dr. Nickolas Ijumaa hii.
“Himid amekuwa akicheza na maumivu makali katika goti la kulia na tulimzuia kucheza mechi baada ya mechi mbili zilizoita baada ya kuona yale maumivu yanaendelea na tulifanya vipimo vya M.R.I ambavyo vilionyesha kuna hitilafu kwenye goti lake na alipata matibabu katika Hospitali ya Moi (Muhimbili).
“Lakini baada ya kupata matibabu takribani wiki moja tuliamua ni busara zaidi kumpeleka katika Hospitali ya Vincent Pallotti nchini Afrika Kusini kwenda kuangaliwa zaidi ukiangalia Himid bado ana majukumu ya klabu na makubwa ya timu ya Taifa vilevile kama nahodha,” alisema.
Wazir upasuaji
Katika hatua nyingine, Mwankemwa alithibitisha kuwa mshambuliaji wa timu hiyo, Wazir Junior, anatarajiwa kufanyiwa upasuaji mdogo wa mguu Moi baada ya donge la damu kuvilia chini ya mguu.
“Wazir (Junior) alikuwa na tatizo kwenye kifundo cha mguu na tumemfanyia vipimo vyote vya M.R.I, X-Ray, alikuwa akitibiwa Moi sasa hivi taratibu zinafanyika matibabu ya zaidi yatakuwa katika Hospitali ya Moi, ambayo atafanyiwa upasuaji mdogo baada ya kujulikana kuwa chini ya mguu kuna bonge la damu kwa hiyo tunatarajia ndani ya siku mbili hizi Junior kufanyiwa upasuaji huo,” alisema.
Amoah uchunguzi
Akizungumzia matibabu ya beki Daniel Amoah, anayesumbuliwa na maumivu ya goti, alisema kuwa wanatarajia kufanya taratibu za kumfanyia kipimo cha M.R.I na kuangalia tatizo linalomkabili ndani ya goti hilo.
“Mtakumbuka siku ya mechi yetu na Stand United alianguka kandokando ya kiwanja na kujiumiza lakini tulikuwa tukimuuguza na kumpatia madawa akapata nafuu akacheza mechi ya Simba, lakini baada ya mechi ya Simba yale maumivu yamejirudia tena na sasa tunafanya taratibu za kumfanyia kipimo cha M.R.I…na baada ya kupata majibu ya M.R,I tutawafahamisheni zaidi ni jinsi gani matibabu yake yatakuaje,” alisema.