KLABU Bingwa ya Afrika Mashariki na Kati, Azam FC, imefanikiwa kutoka sare ya bao 1-1 dhidi ya Kagera Sugar, katika mchezo wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara (VPL) uliomalizika Uwanja wa Kaitaba, mjini Bukoba, Kagera jioni ya leo.

Matokeo hayo yameifanya Azam FC kufikisha jumla ya pointi 34 katika nafasi ya tatu kwenye msimamo sawa na Yanga iliyo nafasi ya pili kwa uwiano mzuri wa mabao ya kufunga na kufungwa huku ikiwa na mchezo mmoja mkononi sawa na Simba, ambayo ipo kileleni kwa pointi 41.

Mchezo ulikuwa mkali na wa aina yake, ilishuhudiwa timu zote mbili zikijipatia mabao yake kipindi cha pili huku Azam FC ikitengeneza nafasi nyingine takribani tatu lakini haikuweza kuzitumia vema.

Kagera Sugar ndio iliyoanza kupata bao la uongozi dakika ya 50 akimalizia mpira wa adhabu ndogo uliopigwa na Jaffary Kibaya, lakini dakika tatu baadaye Azam FC ilisawazisha kwa bao safi kabisa la kiufundi lililopigwa na winga Idd Kipagwile, aliyeingia kipindi cha pili kuchukua nafasi ya Mbaraka Yusuph.

Bao hilo alilofunga Kipagwile kufuatia pasi ya mshambuliaji Shaaban Idd, limemfanya kuandika bao lake la kwanza msimu huu kwenye mechi za ligi.

Mara baada ya mchezo huo, kikosi cha Azam FC kinatarajia kuondoka mjini Bukoba kesho Jumanne saa 3 asubuhi kwa Ndege ya Shirika la Tanzania (ATCL) kurejea Dar es Salaam, tayari kuanza safari nyingine Jumatano hii alfajiri kuelekea mkoani Iringa kukabiliana na Lipuli mtanange utakaopigwa Uwanja wa Samora Ijumaa hii.

Kikosi cha Azam FC leo:

Razak Abalora, Swaleh Abdallah/Enock Atta dk 46, Bruce Kangwa, David Mwantika, Yakubu Mohammed (C), Abdallah Kheri, Stephan Kingue/Paul Peter dk 74, Frank Domayo, Salmin Hoza, Mbaraka Yusuph/Idd Kipagwile dk 46 na Shaaban Idd