KLABU Bingwa ya Afrika Mashariki na Kati, Azam FC, inatarajia kuondoka jijini kesho Jumapili asubuhi kwa ndege, tayari kabisa kuelekea mkoani Kagera, Bukoba kukabiliana na Kagera Sugar kwenye Uwanja wa Kaitaba keshokutwa Jumatatu.

Azam FC inaelekea mkoani humo kwa kazi moja tu ya kusaka ushindi ili kujiweka vema kwenye msimamo wa ligi baada ya kuteleza katika mchezo uliopita ikifungwa na Simba bao 1-0.

Tayari kikosi hicho kimeshaanza maandalizi kujiandaa na mchezo huo, kikianza mazoezi jana Ijumaa na leo kikitarajia kujifua kwa mara ya mwisho kabla ya kuelekea mkoani humo, ambapo mara mwisho msimu uliopita iliifunga Kagera Sugar mabao 3-2.

Mabingwa hao wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara (VPL) msimu wa 2013/2014, wataendelea kuikosa huduma ya Nahodha Himid Mao ‘Ninja, aliyepewa mapumziko maalum kufuatia majeraha ya goti la mguu wa kulia yanayomsumbua, pamoja na mshambuliaji Wazir Junior na beki Daniel Amoah, ambao nao ni majeruhi.

Aidha itamkosa nahodha wake msaidizi, Agrey Moris, aliyekusanya kadi tatu za njano, zinazomfanya kukosa mechi moja ijayo, lakini wachezaji wengine wote waliobakia wapo fiti kwa ajili ya mchezo huo, ukiondoa majeruhi wa muda mrefu Joseph Kimwaga, ambaye anaendelea na programu ya mwisho (recovery) ya kurejea dimbani kwenye ushindani.

Mpaka sasa Azam FC imejikusanyia jumla ya pointi 33 kwenye nafasi ya tatu katika msimamo wa ligi ikiwa sawa na Singida United iliyonafasi ya nne, ikizidiwa pointi nane na Simba iliyojikusanyia pointi 41 kileleni huku Yanga ikiwa nafasi ya pili kwa pointi zake 34.