DROO ya raundi ya 16 bora ya michuano ya Kombe la Shirikisho (Azam Sports Federation Cup) imepangwa muda mchache uliopita, ambapo Azam FC imepangwa kucheza ugenini dhidi ya KMC kati ya Februari 22 hadi 25 mwaka huu.

Mchezo huo huenda ukafanyika Uwanja wa Azam Complex au Uhuru, hii itategemeana na uamuzi wa wenyeji KMC watakaochagua uwanja watakaoutumia.

Hii itakuwa ni mara ya pili msimu huu kwa timu hizo mbili kucheza, mara ya kwanza ilikuwa kwenye mchezo maalumu wa kirafiki wa maandalizi ya msimu uliofanyika Azam Complex na Azam FC kushinda bao 1-0, lililofungwa kwa mkwaju wa penalti na Nahodha Msaidizi Agrey Moris baada ya Wazir Junior kufanyiwa madhambi ndani ya eneo la hatari.

Azam FC inayodhaminiwa na Benki ya NMB, Maji safi ya Uhai Drinking Water na Tradegents, wamefika hatua hiyo baada ya kuifunga Shupavu mabao 5-0 kwenye raundi iliyopita, yaliyofunga na mshambuliaji Paul Peter aliyefunga hat-trick, Yahya Zayd na Idd Kipagwile.

KMC iliyopanda Ligi Kuu kwa ajili ya msimu ujao, nayo imefuzu kwa kuichapa Toto African ya Mwanza mabao 7-0, mchezo uliofanyika usiku wa kuamkia leo kwenye Uwanja wa Azam Complex.

Bingwa wa michuano hiyo mbali kubeba kombe, medali na kitita cha Sh. Milioni 50, pia ndiye atakayeiwakilisha nchi katika michuano ya Kombe la Shirikisho Afrika mwakani.

Mechi nyingine saba zilizobakia:

-Stand United vs Dodoma FC

-JKT Tanzania vs Ndanda FC

-Kiluvya United vs Tanzania Prisons

-Majimaji vs Young Africans

-Singida United vs Polisi Tanzania

-Njombe Mji vs Mbao FC

-Buseresere FC vs Mtibwa Sugar