KLABU Bingwa ya Afrika Mashariki na Kati, Azam FC, imeshindwa kutamba ugenini baada ya kufungwa bao 1-0 dhidi ya Simba, katika mchezo mkali wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara (VPL) uliofanyika Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam leo jioni.

Matokeo hayo yanaifanya Azam FC kubakia nafasi ya tatu kwenye msimamo wa ligi hiyo ikiwa na pointi 33 sawa na Singida United iliyo nafasi ya nne, ikiwa nyuma ya Yanga iliyojikusanyia pointi 34 katika nafasi ya tatu huku Simba ikijikita kileleni baada ya kufikisha pointi 41.

Azam FC ilianza vema mchezo huo kwa kufanya shambulizi kali dakika ya tano baada ya beki wa kushoto Bruce Kangwa, kuwahadaa mabeki wa Simba na kupiga krosi nzuri iliyomkuta winga Idd Kipagwile, aliyepiga kichwa kilichopaa juu ya lango.

Simba ilipatia bao pekee dakika ya 37 lililofungwa na Emmanuel Okwi, akimalizia kwa shuti la chini kufuatia krosi ya chini aliyopenyezewa na Asante Kwasi.

Safu ya ushambuliaji ya Azam FC kukosa umakini na kupoteza mipira kwa kiasi fulani iliiathiri kipindi cha kwanza, lakini mabadiliko ya kuingia Salum Abubakar ‘Sure Boy’ na kutoka Idd Kipagwile dakika ya 56 yaliiongezea uhai Azam FC na kufanikiwa kutawala mchezo kwa asilimia kubwa kipindi cha pili.

Mshambuliaji wa Azam FC, Shaaban Idd, aliyeingia mwanzoni mwa kipindi cha pili kuchukua nafasi ya Mbaraka Yusuph, kama angekuwa makini huenda angeisawazishia timu hiyo dakika ya 59 baada ya kupokea pasi safi ya Yahya Zayd, lakini shuti alilopiga lilitoka sentimita chache ya lango la Simba.

Kiujumla hadi sasa Azam FC imeshacheza mechi 17 za ligi hiyo, imeshinda mechi tisa, sare sita na kupoteza mechi mbili huku ikiwa imefunga jumla ya 19 na kuruhusu nyavu zake kuguswa mara nane.

Mara baada ya mchezo huo, kikosi cha Azam FC kinatarajia kupumzika kesho Alhamisi kabla ya kurejea tena mazoezini Ijumaa jioni tayari kuanza maandalizi ya kuikabili Kagera Sugar katika mtanange wa ligi utakaofanyika Uwanja wa Kaitaba, Bukoba Jumatatu ijayo.

Kikosi cha Azam FC leo jioni:

Razak Abalora, Daniel Amoah, Bruce Kangwa, Yakubu Mohammed, Agrey Moris, Stephan Kingue, Idd Kipagwile/Salum Abubakar dk 56, Frank Domayo, Mbaraka Yusuph/Shaaban Idd dk 46, Yahya Zayd/Bernard Arthur dk 71, Enock Atta-Agyei