KLABU Bingwa ya Afrika Mashariki na Kati, Azam FC, imeendeleza dozi nene kwenye michuano ya Kombe la Shirikisho (Azam Sports Federation Cup) baada ya kuichapa Shupavu mabao 5-0, mchezo uliomalizika jioni ya leo Jumanne kwenye Uwanja wa Jamhuri, Morogoro.

Hii ni mara ya pili inaibuka na ushindi mnono kwenye michuano hiyo baada ya mechi ya awali kuichapa Area C United ya Dodoma mabao 4-0.

Katika mchezo huo, benchi la ufundi la Azam FC lilikifanyia marekebisho kikosi cha timu hiyo tofauti na kila kilichoanza kwenye mchezo wa mwisho dhidi ya Yanga.

Mshambuliaji kinda Paul Peter, alijiandikia rekodi ya aina yake tokea apandishwe timu hiyo baada ya kufunga hat-trick yake ya kwanza iliyochagiza ushindi huo mnono wa Azam FC.

Mbali na Peter, pia kulikuwa na kiwango vizuri kwa wachezaji wa Azam FC akiwemo winga Idd Kipagwile, mshambuliaji Yahya Zayd, Frank Domayo, mabeki Abdallah Kheri, David Mwantika na kipa Mwadini Ally, ambao waliukosa mchezo uliopita.

Bao la kwanza la Azam FC limeweka kimiani na Yahya Zayd dakika ya 44 kwa mkwaju wa penalti baada ya winga Idd Kipagwile, kuangushwa ndani ya eneo la 18.

Kipagwile akaipeleka mapumziko Azam FC kwa uongozi wa mabao 2-0, baada ya kutupia bao safi la pili akimtesa vilivyo kipa wa Shupavu.

Kipindi cha pili Azam FC iliongeza nguvu kwenye ushambuliaji kwa kumpumzisha Mbaraka Yusuph na kuingia Peter aliyemalizia mabao matatu ya nguvu dakika ya 56, 77 na 87.

Kwa matokeo hayo, Azam FC imesonga mbele kwa raundi ya 16 bora na kwa sasa inasubiria kupangiwa mpinzani wake.

Kikosi hicho kinachodhaminiwa na Benki ya NMB, Maji Safi ya Uhai Drinking Water, Tradegents, kinatarajia kurejea jijini Dar es Salaam kesho asubuhi tayari kabisa kwa maandalizi ya mchezo ujao wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara (VPL) dhidi ya Ndanda utakaofanyika Uwanja wa Azam Complex Jumamosi hii saa 1.00 usiku.

Kikosi cha Azam FC:

Mwadini Ally, David Mwantika, Bruce Kangwa, Yakubu Mohammed/Daniel Amoah dk 81, Abdallah Kheri, Frank Domayo, Idd Kipagwile, Salmin Hoza/Abdallah Masoud dk 67, Mbaraka Yusuph/Paul Peter dk 46, Yahya Zayd, Ramadhan Singano