KIPA wa Klabu Bingwa ya Afrika Mashariki na Kati Azam FC, Razak Abalora, ametwaa Tuzo ya Mchezaji Bora wa timu hiyo (NMB Player Of The Month) mwezi Desemba-Januari.

Razak anakuwa mchezaji wanne kutwaa tuzo hiyo  iliyoanzishwa na uongozi wa timu hiyo msimu huu, ya kwanza akiitwaa beki Yakubu Mohammed (Agosti-Septemba), Mbaraka Yusuph akabeba ya pili (Septemba-Oktoba) kabla ya Nahodha Himid Mao ‘Ninja’, kuitwaa iliyopita (Oktoba-Novemba).

Kipa huyo aliyeiongoza Azam FC kutwaa ubingwa wa Kombe la Mapinduzi mwaka huu kwa mara ya pili mfululizo, ametwaa tuzo hiyo baada ya kujizolea kura 116 sawa na asilimia 49.6 ya kura zote 234 zilizopigwa akiwazidi beki Bruce Kangwa na Yahya Zayd ambao waligawana kura 118 zilizobakia kwa kila mmoja kupata 59 (sawa na asilimia 25.2 kwa kila mmoja).

Tuzo hiyo inatolewa na wadhamini wakuu wa Azam FC, Benki bora kabisa nchini ya NMB, ambayo mwanzoni mwa wiki hii imeiongezea mkataba wa udhamini timu hiyo kwa kipindi kingine cha mwaka mmoja.

Zayd atwaa ile ya Uhai

Wakati Razak akipata mafanikio hayo, Yahya Zayd naye amefanikiwa kubeba Tuzo ya Mchezaji Bora wa Mwezi wa timu ya Vijana ya Azam FC (Uhai Player Of The Month) baada ya kuwa na mchango mkubwa kwenye timu kubwa ya matajiri hao.

Zayd tokea apandishwe msimu huu, amekuwa na msaada mkubwa kwenye timu kubwa msimu huu hadi sasa akiwa amefunga mabao mawili katika Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara (VPL) huku akitoa pasi tatu zilizozaa mabao.

Wadhamini namba mbili wa Azam FC, maji safi ya Uhai Drinking Water ndio wanaotoa tuzo hiyo, ambapo mpaka sasa imeshakuchukuliwa na wachezaji watatu, Twaha Rajab akianza kuibeba (Agosti-Septemba), Paul Peter akafuatia (Septemba-Oktoba) huku ya mwisho akiichukua mshambuliaji aliyeko kwa mkopo Coastal Union, Andrew Simchimba (Oktoba-Novemba).