REKODI ya Azam FC ya kutofungwa kwenye mechi 14 mfululizo za Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara (VPL), imefikia tamati jioni ya leo baada ya kufungwa na Yanga mabao 2-1, mchezo uliofanyika Uwanja wa Azam Complex, Chamazi, Dar es Salaam.

Katika mechi hizo ambazo haijapoteza, Azam FC imeshinda mechi nane na kutoka sare sita, ambapo kwa matokeo hayo imebakiwa na pointi zake 30 baada ya kucheza mechi 15 ikiwa imemaliza raundi ya kwanza.

Azam FC ndio ilikuwa ya kwanza kuliona lango la Yanga dakika ya nne tu, kwa bao safi la mshambuliaji Shaaban Idd, aliyetumia vema krosi ya chini ya beki wa kushoto Bruce Kangwa, aliyempiga chenga Hassan Kessy.

Yanga ikarejea mchezoni na kupata ushindi kwa mabao ya Obrey Chirwa dakika ya 30 na Gardiel Michael dakika ya 43, yaliyodumu hadi kumalizika kwa mchezo huo.

Mabingwa hao wa ligi msimu 2013/2014 walimaliza pungufu katika mchezo huo baada ya kiungo Salum Abubakar ‘Sure Boy’, kuonyeshwa kadi nyekundu dakika ya 81 kufuatia kumsukuma Kessy.

Mara baada ya mchezo huo, kikosi cha Azam FC kinatarajia kuelekea mkoani Morogoro kesho Jumapili mchana tayari kabisa kupambana na Shupavu ya huko katika mchezo wa raundi ya tatu ya Kombe la Shirikisho (Azam Sports Federation Cup) utakaofanyika Uwanja wa Jamhuri Jumanne ijayo saa 8.00 mchana.

Kikosi Azam FC leo:

Razak Abalora, Himid Mao (C), Bruce Kangwa, Yakubu Mohammed, Agrey Moris, Stephan Kingue/Mbaraka Yusuph dk 54, Joseph Mahundi, Salum Abubakar, Bernard Arthur/Salmin Hoza dk 36, Shaaban Idd/Paul Peter dk 65