WACHEZAJI watatu wa Azam FC, kipa Razak Abalora, beki Bruce Kangwa na mshambuliaji Yahya Zayd, wamechaguliwa kuwania Tuzo ya Mchezaji Bora wa mwezi wa NMB (NMB Player of the Month) Desemba-Januari.

Tuzo hiyo inatolewa na wadhamini wakuu wa Azam FC, Benki ya NMB ambao wametoka kuongeza mkataba mpya wa mwaka mmoja jana, ulioifanya kuendelea kuwadhamini mabingwa hao kwa msimu wa nne mfululizo tangu 2014/2015.

Nyota hao wanaingia kwenye kinyang’anyiro hicho baada ya kufanya vizuri kwa miezi hiyo miwili, wakiiongoza Azam FC kutwaa taji la Kombe la Mapinduzi mwaka huu kwa mara ya pili mfululizo pamoja na kuisaidia katika mbio zake za kuwania ubingwa wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara (VPL).

Tuzo hiyo itatolewa kwa mshindi Jumamosi hii wakati Azam FC ikivaana na Yanga kwenye mchezo wa ligi utakaofanyika Uwanja wa Azam Complex saa 10.00 jioni.

Mpaka sasa wachezaji watatu wameshaitwaa tokea ianzishwe msimu huu, ya kwanza akiibeba beki Yakubu Mohammed (Agosti-Septemba), mshambuliaji Mbaraka Yusuph (Septemba-Oktoba), nahodha Himid Mao ‘Ninja’ (Oktoba-Novemba).

Ukiwa kama shabiki wa soka unaweza kuanza kupiga kura yako miongoni mwa wachezaji hao watatu kwa kubofya kwenye linki hii:  https://poll.fbapp.io/nmb-player-of-the-month-december-january