KOCHA Mkuu wa Azam FC, Aristica Cioaba, ameonekana kuwa mjanja kwenye mbio za ubingwa wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara (VPL) baada ya kujiwekea mikakati ya kutopoteza mchezo wowote.

Kauli hiyo ameitoa jana mara baada ya kuinyuka Tanzania Prisons mabao 2-0 katika mchezo wa ligi uliofanyika Uwanja wa Sokoine, jijini Mbeya, akidai kuwa ushindi huo umetokana na kuijua vilivyo timu hiyo baada ya kuisoma na kuwapa mbinu wachezaji wake zilizozaa ushindi huo.

“Ilikuwa ni ngumu baada ya kutoka kupata sare mchezo uliopita (Majimaji), pia ilikuwa ngumu katika morali ya wachezaji lakini siku hizi mbili hadi tunacheza niliongea vizuri na wachezaji na kuwaangalia vilivyo wapinzani wetu Tanzania Prisons na nilikuwa najua kila kitu chao.

“Wachezaji wakanielewa na nikawapa mbinu walipoingia uwanjani na wakaziheshimu na kushinda mchezo, wachezaji wengine walikuwa na kadi mbili za njano kama vile Bruce (Kangwa), Enock (Atta) sikutaka kuwapanga matatizo kwa kuwa nawahitaji mchezo ujao (vs Yanga), nawapongeza sana wachezaji wameheshimu mbinu na ksuhinda mchezo,” alisema Aristica Cioaba.

Kocha huyo aliyerejea benchi jana baada ya kumaliza adhabu yake ya kutokaa benchi mechi tatu, alisema kuwa anakiamini kikosi chake kitapambana kwa ajili ya nafasi ya kwanza.

“Nakiamini kikosi changu kitapambana kwa ajili ya nafasi ya kwanza, Simba inamoja ya mpinzani wa nguvu, mimi kocha na timu ya Azam FC,” alisema.

Kuelekea mechi na Yanga 

Akizungumzia mchezo ujao dhidi ya Yanga, Cioaba alisema Yanga ni moja ya timu kubwa nchini ikitoka kutwaa ubingwa wa ligi msimu uliopita na kudai kuwa wataingia uwanjani na kuonyesha umakini mkubwa.

“Mechi itakuwa Chamazi, hautakuwa mchezo mwepesi nitakuwa na muda wa siku tatu wa maandalizi kwa kuwa nina safari ndefu sana na wachezaji wanauchovu kidogo lakini siku hizo tatu nitawaunganisha vema wachezaji na kujaribukufanya vizuri dhidi ya Yanga Chamazi, sihitaji kupoteza mchezo wowote hapo baadaye,” alisema.

Azam FC itacheza na Yanga Jumamosi hii, mchezo utakaofanyika Uwanja wa Azam Complex saa 1.00 usiku kwa mujibu wa ratiba inavyoonyesha.

Hadi sasa ikiwa imecheza mechi 14 za ligi, Azam FC imefanikiwa kuwa rekodi bora baada ya kutopoteza mchezo hata mmoja, ikiwa imeshinda mechi nane na sare sita ikiwa kileleni kwa pointi zake 30 ikiizidi mechi moja Simba ambayo ipo nafasi ya pili ikijikusanyia 29.