KLABU Bingwa ya Afrika Mashariki na Kati, Azam FC, imedhihirisha kuwa inautaka ubingwa wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara (VPL) baada ya jioni ya leo kupata ushindi mujarabu wa ugenini mkoani Mbeya ikiichapa Tanzania Prisons mabao 2-0.

Ushindi huo umeifanya Azam FC kupaa kileleni mwa msimamo wa ligi baada ya kufikisha jumla ya pointi 30 ikiizidi Simba pointi moja ambayo ina mchezo mmoja mkononi itakaoucheza kesho dhidi ya Kagera Sugar.

Azam FC ilibidi isubiri hadi kipindi cha pili kuweza kuandika ushindi huo muhimu kupitia mabao safi ya Yahya Zayd dakika ya 72 kwa kichwa akimalizia mpira wa kona uliochongwa na kiungo Salmin Hoza, na la mwisho likishindiliwa kimiani kiufundi na chipukizi Paul Peter dakika ya 83 aliyepokea pasi safi ya Zayd.

Mabadiliko ya kuongeza nguvu kwenye kiungo baada ya kuingia Hoza na mshambuliaji Peter, kwa kiasi fulani yaliongeza kasi ya mashambulizi na kuwachanganya wachezaji wa Tanzani Prisons, hali iliyopelekea Azam FC kupata mabao hayo yaliyozidi kuchochea mbio zao za kuwania ubingwa.

Huo ni ushindi wa pili mfululizo kihistoria kwa Azam FC kwenye uwanja huo dhidi ya Prisons katika mechi nane walizocheza huku mabingwa hao wakipoteza mara mbili na mechi nne zikiisha kwa sare.

Kihistoria mchezo huo ulikuwa ni wa 15 kwa timu hizo kukutana kwenye ligi, Azam FC ikiwa na rekodi bora ya ushindi ikifanya hivyo mara sita, Prisons ikiibuka kidedea mara tatu na mechi sita zikiisha kwa sare.   

Aidha Azam FC imefanikiwa kuondoka na pointi nne katika mechi zake mbili za ugenini kufuatia sare ya bao 1-1 dhidi ya Majimaji Alhamisi iliyopita na ushindi wa leo ilipokipiga na maafande hao.

Mara baada ya mchezo huo, kikosi cha Azam FC kinatarajia kuondoka jijini Mbeya kesho Jumatatu alfajiri kurejea Dar es Salaam tayari kujiandaa na mchezo ujao wa ligi dhidi ya Yanga utakaofanyika Uwanja wa Azam Complex Januari 27, mwaka huu.

Kikosi cha Azam FC leo:

Razak Abalora, David Mwantika, Abdallah Kheri/Hoza dk dk 73, Agrey Moris, Yakubu Mohammed, Stephan Kingue, Himid Mao (C), Salum Abubakar, Joseph Mahundi, Shaaban Idd/Paul Peter dk 73, Yahya Zayd/Idd Kipagwile dk 85