MSIMU uliopita Klabu Bingwa ya Afrika Mashariki na Kati, Azam FC, ilifanya maajabu kwa kujiandikia historia baada ya kupata pointi tatu kwa mara ya kwanza dhidi ya Tanzania Prisons kwenye Uwanja wa Sokoine, jijini Mbeya.

Azam FC itaingia tena ndani ya uwanja huo kesho Jumapili kusaka ushindi dhidi ya maafande hao wa magereza, na kuendeleza rekodi hiyo kwa mara ya pili mfululizo kwenye Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara (VPL).

Kikosi hicho kinachodhaminiwa na Maji safi ya Uhai Drinking Water, Benki ya NMB na Tradegents, kipo vizuri kabisa kuelekea mchezo huo na wachezaji wanamorali ya hali ya juu ya kuhakikisha wanaibuka na ushindi.

Azam FC itaingia dimbani ikiwa na kumbukumbu ya kutoka sare ya bao 1-1 ugenini dhidi ya Majimaji kwenye mchezo uliopita huku Prisons wakitoka kuifunga Mbeya City mabao 3-2 katika mchezo wa mahasimu wa jiji la Mbeya ‘Mbeya Derby’.

Akizungumza kuelekea mtanange huo muhimu kabisa kwa matajiri hao viunga vya Azam Complex katika kampeni yake ya mbio za ubingwa, Kocha Mkuu Aristica Cioaba, alisema kuwa wanaingia kwenye mchezo huo kwa kazi moja tu ya kuhakikisha wanaibuka na ushindi.

“Naingia kwenye mchezo huu wa Tanzania Prisons nikiwa najiamini, sijapoteza mechi hata moja nimecheza mechi 13 za ligi na sijapoteza mchezo hata mmoja na kesho nataka kuendeleza rekodi nzuri tuliyoanza nayo hadi sasa, nimeongea na wachezaji kwa kuwapa morali na kuwaambia wasahau yaliyotokea kwenye mechi iliyopita.

“Lakini napenda kuongea na mashabiki na baadhi ya watu kuwa ukitaka kutwaa ubingwa hautakiwi kuwa na safari ndefu kama hizi kutokana na uchovu kwa wachezaji, nimetoka kwenye Kombe la Mapinduzi na moja kwa moja tulikwenda Songea wachezaji wakiwa wamechoka kutokana na safari ndefu ya takribani saa 19 na bado tumekuja Mbeya kwa safari nyingine ndefu, hii kwa kiasi fulani inawachosha wachezaji,” alisema.

Alisema tatizo kubwa lililoko kwenye timu yake kuelekea mchezo wa kesho ni wachezaji wake watatu muhimu kuwa na kadi mbili za njano huku akiweka wazi kuwa atawapumzisha kutokana na kukabiliwa na mchezo dhidi ya Yanga Januari 27 mwaka huu.

“Sitaki kuwaweka kwenye hatari, najua soka la Tanzania kuwa waamuzi wanaweza kutoa kadi za njano nyingine kwa haraka, siwezi kuwaweka kwenye mchezo wa kesho na nawatunza kuelekea mchezo dhidi ya Yanga, nitawaingiza baadhi ya wachezaji kikosini na naamini wataingia uwanjani na kucheza vizuri na kupambana na kuisaidia timu kupata pointi zote, sijaja hapa kwa ajili ya sare nimekuja kushinda,” alisema.

Aidha Azam FC itaendelea kuwakosa wachezaji wake wawili beki Daniel Amoah, mshambuliaji Mbaraka Yusuph, ambao wanaendelea na programu ya mwisho ya kurejea uwanjani baada ya kupona majeraha yao, wachezaji hao pamoja na wale waliobakishwa Dar es Salaam kwa pamoja wanafanya mazoezi na kikosi cha timu ya Vijana ya Azam FC ‘Azam U-20’ chini ya Kocha Mkuu, Meja MStaafu Abdul Mingange.

Rekodi zilipokutana

Mpaka sasa kihistoria timu hizo zimekutana mara 14 kwenye mechi za ligi, Azam FC ikiwa na rekodi ya kushinda mara tano, Prisons yenyewe mara tatu ikiibuka kidedea huku ikishuhudiwa mechi sita zikiisha kwa sare.

Azam FC ambayo inauchukulia kwa uzito mkubwa mchezo huo hasa ikitaka kuifikia Simba kwenye mbio za ubingwa, ilipata ushindi wa bao 1-0 kwenye mchezo wa mwisho uliofanyika uwanjani hapo msimu uliopita.

Bao pekee la Azam FC lilifungwa kiustadi kwa shuti na aliyekuwa kiungo mkabaji wa timu hiyo, Michael Bolou, bao lililofanya rekodi kuandikwa upya kwa mabingwa hao kupata ushindi wa kwanza Sokoine dhidi ya Prisons kwenye mechi saba walizocheza ndani ya dimba hilo.

Ukiondoa mechi moja ambayo Azam FC imeitambia Prisons, mechi nyingine sita zilizobakia zilizopigwa mjini Mbeya, maafande hao wameshinda mara mbili huku nne zikiisha kwa sare.

Jumla ya mabao 22 yamefungwa na timu hizo katika mechi zote 14 walizokutana, Azam FC imefunga 12 (nusu ya mabao yote) na Prisons ikitupia 10 tu kwenye nyavu za mabingwa hao wa ligi msimu 2013/2014.

Ushindi wowote kesho utaifanya Azam FC kufikisha jumla ya pointi 30 kwenye msimamo wa ligi na kukaa kileleni kwa muda ikisubiria matokea ya Simba itakayocheza na Kagera Sugar katika Uwanja wa Kaitaba keshokutwa Jumatatu.