BAADA ya kutoka kutwaa ubingwa wa Kombe la Mapinduzi wiki iliyopita, kikosi cha Azam FC kesho Alhamisi kitakuwa kibaruani kusaka pointi tatu muhimu dhidi ya Majimaji kwenye mchezo wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara (VPL) utakaoanza saa 8.00 mchana.

Tayari kikosi cha Azam FC kimewasili mjini Songea, Ruvuma tokea jana usiku tayari kwa mpambano huo, ambapo wachezaji wote wako vizuri kabisa na wanamorali ya hali ya juu kuhakikisha wanaibuka na pointi zote tatu.

Kuelekea mtanange huo, kikosi cha timu leo saa 8 mchana kimefanya mazoezi ya mwisho kwenye Uwanja wa Majimaji, utakaochezewa mchezo huo, ambapo wachezaji walionekana kufanya vema na kusikiliza kwa makini maelekezo yote ya benchi la ufundi chini ya Mromania, Aristica Cioaba.

Kocha, nahodha ni pointi ushindi

Akizungumza mara baada ya kumalizika kwa mazoezi hayo, Kocha Cioaba alisema kuwa licha ya uwanja kutokuwa kwenye hali nzuri watahakikisha wanapambana na kuzoa pointi zote tatu.

“Mechi itakuwa ngumu kwa kuwa mechi zote za nje ya Chamazi (Azam Complex) zinakuwaga ngumu hasa kutokana na uwanja, lakini Azam FC ina wachezaji wanaojua kucheza mpira hivyo kesho kinachohitajika kwao ni kuuzoea uwanja, kuweka umakini, kumuheshimu mpinzani na kupambana kwa hali ya juu kuhakikisha wanazoa pointi zote tatu,” alisema.

Alisema wachezaji wote wako tayari kwa mchezo huo, isipokuwa Daniel Amoah, aliyerejea kutoka majeruhi na baadhi ya wachezaji waliobakia Dar es Salaam, na kudai wale wote walioonekana kwenye michuano ya Kombe la Mapinduzi wako tayari kucheza kesho.

“Mechi zote ni muhimu kwetu sisi kwa kuwa ukitaka kukaa kileleni unatakiwa kukusanya pointi zote za ugenini, huu ni mpira na kila mmoja anapaswa kulijua hilo, naiamini timu yangu, moyo wa kujitolea upo hapa, morali ipo kikosini baada ya Kombe la Mapinduzi na naiamini timu kesho itaingia uwanjani kwa hamasa na kuzoa pointi zote, najua ni mechi ngumu, uwanja sio mzuri, lakini wapinzani nao wanacheza kwenye uwanja huu huu,” alisema.

Naye Nahodha Himid Mao ‘Ninja, alisema kuwa wao kama wachezaji wamemaliza vema maandalizi kuelekea mchezo huo huku akidai mechi hiyo kuwa mchana haitawaathiri chochote na kuahidi wachezaji wote kupambana kwa ajili ya pointi tatu.

“Morali ilikuwepo vizuri kwenye maandalizi yetu ya mwisho, hali ya hewa ya hapa sidhani kama ni mbaya sana, japo hatujacheza mechi saa nane, lakini sisi kama wanajeshi, mechi imeshapangwa hivyo hatuna jinsi lazima tucheze vyovyote itakavyokuwa kwa hiyo naamini mimi, wachezaji wenzangu tutapambana kadiri tunavyoweza kutetea pointi tatu ambazo tunatakiwa kuzipata hapa,” alisema.

Mwenendo wa timu zote  

Azam FC inayodhaminiwa na Maji Safi ya Uhai Drinking Water, Benki ya NMB na Tradegents, imekuwa na msimu mzuri hadi sasa ikielekea raundi ya 13 ambapo katika mechi 12 za awali ilizocheza za ligi, imefanikiwa kushinda mechi saba na sare tano ikiwa haijapoteza mchezo hata mmoja, ikijikusanyia pointi 26 kwenye nafasi ya pili sawa na Simba iliyo kileleni kwa tofauti ya mabao ya kufunga na kufungwa.

Majimaji ipo nafasi ya 13 kwenye msimamo baada ya kujikusanyia jumla ya pointi 11 zilizotokana na ushindi wa mechi mbili, sare tano na kupoteza sita huku katika mechi zake tano zilizopita ikishinda mara mbili, sare mbili na kutoka sare moja.

Rekodi zao (Head to Head)

Azam FC kihistoria imekutana mara nane na Majimaji kwenye mechi za ligi, Azam FC ikishinda asilimia 98 ya mechi hizo yaani tano, Majimaji ikiwa haijawahi kuonja pointi tatu dhidi yao huku ikishuhudiwa mechi tatu zikienda sare.

Mara ya mwisho timu hizo kukutana ndani ya uwanja huo ilikuwa ni Desemba mwaka juzi, ambapo timu hizo zilitoka sare ya bao 1-1, bao la Azam FC likifungwa na aliyekuwa mshambuliaji wa timu hiyo, Yahaya Mohammed na Majimaji ikisawazsiha kupitia kwa Alex Kondo.