BAADA ya safari ndefu ya takribani saa 18, hatimaye kikosi cha Klabu Bingwa ya Afrika Mashariki na Kati, Azam FC, kimewasili salama mkoani Ruvuma, Songea muda mchache uliopita.

Azam FC imewasili kwa kazi moja ya kuhakikisha inavuna ushindi kwenye mchezo wake wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara (VPL) dhidi ya Majimaji ya huku utakaofanyika Uwanja wa Majimaji keshokutwa Alhamisi saa 8.00 mchana.

Mabingwa hao wametua Songea na baadhi ya wachezaji walioshiriki michuano ya Kombe la Mapinduzi wiki iliyopita na kuibuka mabingwa kwa mara ya pili mfululizo, taji ambalo kihistoria inaongoza kulitwaa ikiwa imelibeba mara nne.

Kikosi hicho bado kitaendelea kuwakosa wachezaji wake wawili, beki Daniel Amoah na mshambuliaji Mbaraka Yusuph, ambao hawako kwenye programu ya mechi mbili za Nyanda za Juu Kusini, ikiwa ya pili dhidi ya Tanzania Prisons itakayofanyika Uwanja wa Sokoine, Mbeya Jumapili hii.

Shangwe za mashabiki zaibuka

Wakati kikosi hicho kikiwa njiani kabla ya kuwasili Songea, kimekutana na shangwe kubwa za mashabiki mabalimbali wa soka waliokuwa wakiwashangilia wachezaji hasa Masasi, mkoani Mtwara walipoenda kupata chakula cha mchana.

Mashabiki hao walionekana kuwashangilia wachezaji kwa kupiga nao picha na kuwagusa kutokana na kazi kubwa wanayoendelea kuifanya msimu huu huku Nahodha Himid Mao ‘Ninja’, beki Yakubu Mohammed, Salum Abubakar ‘Sure Boy’, Agrey Moris, Razak Abalora na Frank Domayo wakipata shangwe za kutosha kutoka kwa mshabiki hao.

Baada ya kikosi hicho kuwasili, kinatarajia kupumzika hadi kesho Jumatano mchana kitakapofanya mazoezi ya mwisho kwenye uwanja wa mechi kabla ya Alhamisi kupamabana na Majimaji katika mchezo unaosubiriwa kwa hamu kubwa na wakazi wa mjini Songea.

Azam FC inayodhaminiwa na Maji Safi ya Uhai Drinking Water, Benki bora nchini ya NMB na Tradegents, hadi sasa inashika nafasi ya pili kwenye msimamo wa ligi ikiwana pointi 26 sawa na Simba iliyokileleni kwa tofauti ya mabao ya kufunga na kufungwa.