MARA baada ya kutwaa ubingwa wa Kombe la Mapinduzi jana, kikosi cha Klabu Bingwa ya Afrika Mashariki na Kati Azam FC, kesho Jumatatu asubuhi kitaanza safari ya kuelekea kwenye mikoa ya Nyanda za Juu Kusini kucheza mechi mbili muhimu za Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara (VPL).

Azam FC imetwaa ubingwa wa nne wa Kombe la Mapinduzi baada ya kuichapa URA ya Uganda kwa mikwaju ya penalti 4-3 baada ya dakika 90 kumalizika kwa suluhu na tayari kikosi hicho leo mchana kimerejea jijini Dar es Salaam kwa mapumziko mafupi kabla ya kesho kuanza safari nyingine.

Msafara wa Azam FC uliokuwa ukiongozwa na  na Ofisa Mtendaji Mkuu, Abdul Mohamed na Makamu Mwenyekiti, Abdulkarim Amin ‘Popat’, umepokelewa na mamia ya mashabiki waliojaa bandarini na kuipokea kwa shangwe kubwa kwa furaha.

Azam FC kikiwa katika mikoa hiyo miwili ya Nyanda za Juu Kusini, Ruvuma na Mbeya, kitacheza mechi mbili dhidi ya Majimaji ya mjini Songea itakayofanyika Alhamisi Ijayo saa 8.00 mchana huku ikimalizia mtihani wa mwisho Januari 22 kwa kukipiga na Tanzania Prisons kwenye Uwanja wa Sokoine jijini Mbeya saa 10.00 jioni.

Kikosi cha Azam FC kimerejea kikiwa kwenye hali nzuri na morali ya hali ya juu baada ya kufanya vizuri kwenye Kombe la Mapinduzi, ambapo hadi sasa mchezaji pekee ambaye ni majeruhi ni Mbaraka Yusuph, anayetarajia kuanza mazoezi na wenzake muda wowote kuanzia sasa tayari kumalizia programu ya mwisho ya kurejea uwanjani.

Hadi ligi hiyo inasimama kupisha michuano hiyo iliyofanyika visiwani Zanzibar, kikosi cha Azam FC kina pointi sawa na Simba kileleni kwa msimamo kila mmoja akiwa na pointi 26, timu zote zikiwa kwenye mbio kali za kuwania ubingwa huo.