NI wazi sasa imejulikana usiku huu kuwa, Klabu Bingwa ya Afrika Mashariki na Kati Azam FC, itacheza na Singida United kwenye mchezo wa nusu fainali ya michuano ya Kombe la Mapinduzi, utakaofanyika Uwanja wa Amaan, Zanzibar keshokutwa Jumatano saa 2.15 usiku.

Ukiachana na mtanange huo, nusu fainali ya kwanza itakuwa kati ya URA ya Uganda itakayochuana na Yanga, mchezo utakaofanyika kuanzia saa 10.30 jioni, na washindi wa nusu fainali hizo watafuzu kwa fainali itakayopigwa Jumamosi hii saa 2.15 usiku.

Hii ni mara ya kwanza kwa bingwa huyo mtetezi wa michuano hiyo, kukutana na Singida kwenye michuano hiyo, ambapo itakumbukwa walipocheza katika mchezo wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara (VPL), timu hizo zilitoka sare ya bao 1-1 Oktoba mwaka jana.

Wakati Azam FC inayodhaminiwa na Maji safi ya Uhai Drinking Water, Benki bora nchini ya NMB na Tradegents, ikitinga hatua ya nusu fainali baada ya kushika nafasi ya pili kwenye Kundi A kwa pointi tisa ikizidiwa pointi moja na URA iliyoongoza kundi hilo, Singida yenyewe imeongoza Kundi B kwa pointi 13 sawa na Yanga, iliyoizidi kwa tofauti ya mabao ya kufunga na kufungwa.

Tayari kikosi cha Azam FC kimeshaanza maandalizi ya mchezo huo, leo kilifanya mazoezi saa 9 alasiri na kesho Jumanne kitafanya mengine jioni kabla ya kumenyana na timu hiyo iliyopanda daraja msimu huu na makao makuu yake yakiwa mkoani Singida. 

Mwaka jana Azam FC ilicheza nusu fainali dhidi ya Taifa ya Jang’ombe na kuichapa bao 1-0 lililofungwa kwa shuti la mbali na kiungo Frank Domayo ‘Chumvi’ kabla ya kuingia fainali na kuipiga Simba kipigo kama hicho kupitia bao murua la nahodha Himid Mao ‘Ninja, aliyemtungua kwa mbali aliyekuwa kipa wa wekundu hao, Daniel Agyei.