MARA baada ya kuichapa Simba bao 1-0 na kutinga hatua ya nusu fainali ya michuano ya Kombe la Mapinduzi, Kocha Mkuu wa Azam FC, Aristica Cioaba, amesisitiza kuwa malengo yake ni kutwaa ubingwa huo kwa mara ya pili mfululizo.

Bao pekee la Azam FC limefungwa na winga Idd Kipagwile dakika ya 58 akimalizia pasi safi ya kiungo Frank Domayo, na kuifanya Simba kuendeleza uteja dhidi ya matajiri hao kwa mara ya pili mfululizo baada yam waka jana kupewa kipigo kama hicho kwenye mchezo wa fainali.

Cioaba aliuambia mtandao rasmi wa klabu www.azamfc.co.tz kuwa kwa sasa anapambana kwa ajili ya kutwaa ubingwa na kudai hakuja kutalii kwenye michuano hiyo.

“Unaona kila mmoja amekuja kwenye michuano hii kwa ajili ya kuchukua ubingwa, sijaja hapa kwa ajili mapumziko au kutalii bila kufanya chochote, ndio nitapambana kwa ajili ya ubingwa mechi ijayo (nusu fainali) huenda tukacheza dhidi ya Yanga au Singida United, naziheshimu timu hizi mbili lakini tutaenda kucheza mpira uwanjani, timu itakayocheza mpira mzuri itaweza kushinda mchezo,” alisema.

Mchezo vs Simba 

Akizungumzia mchezo wa dhidi ya Simba, kocha huyo raia wa Romania aliwashukuru wachezaji namna walivyopambana kwenye mchezo huo na kupata ushindi.

“Uliona baada ya mchezo dhidi ya URA wachezaji walihuzunika kwa matokeo na wengine walilia jambo kubwa lilikuwa huenda leo (jana) tungepoteza na tusiingie nusu fainali kwa kuwa Azam ni moja ya timu kubwa na haiwezi kuwa hivi, nikaongea na wachezaji na kuwapa morali nikawaambia bado nawaamini mimi pamoja na uongozi.

“Leo (jana) inatakiwa kupambana ili kila mmoja aone kuwa Azam haijafanya sapraizi bali ipo nafasi ya kwanza kama Simba, kila mmoja anatakiwa kuingia uwanjani leo na kupambana na watu kuona kuwa Azam ina wachezaji wazuri na timu nzuri na inatakiwa kushinda mchezo,” alisema.

Cioaba alisema kuwa wachezaji waliiingia uwanjani na kuheshimu mbinu alizowapa na kila kitu na kudai kuwa anafuraha kubwa na aina ya kikosi alichonacho.

“Umeona ndani ya siku saba nilikuwa na mechi tano, baadhi ya wachezaji wamecheza dakika 90 kwenye mechi tatu na leo walikuwa wamechoka lakini kila mmoja alikuja kwangu na kuniambia kuwa kocha nahitaji kucheza mchezo huu na kupambana katika mchezo huo na kushinda,” alisema.

Kauli kwa mashabiki

Mbali na kuwatakia kheri ya mwaka mpya 2018, kocha huyo amewaahidi zawadi ya moja ya kombe msimu huu mashabiki wa timu hiyo.

“Niliongea huko nyuma kwa mashabiki wa Azam FC kheri ya mwaka mpya kwa mashabiki wote wa Azam FC na familia yote ya Azam na napenda kuongea ya kuwa nitachukua moja ya kombe mwaka huu hapa Azam FC,” alisema.

Azam FC ambayo ni bingwa mtetezi wa michuano hiyo ikidhaminiwa na Maji Safi ya Uhai Drinking Water, Benki ya NMB na Tradegents, itacheza hatua hiyo ya nusu fainali Jumatano ijayo na moja ya timu kati ya Yanga na Singida United, ambazo zitacheza usiku wa leo kuamua hatima hiyo.