KLABU Bingwa ya Afrika Mashariki na Kati, Azam FC, imetinga nusu fainali ya michuano ya Kombe la Mapinduzi kwa staili ya aina yake baada ya kuichapa Simba bao 1-0 usiku huu, mchezo uliofanyika Uwanja wa Amaan, Zanzibar.

Aliyepeleka furaha kwenye viunga vya Azam Complex usiku huu ni winga Idd Kipagwile, aliyewahi kuchezea Simba B kabla ya kutua Majimaji na msimu huu Azam FC, ambaye alifunga bao hilo pekee na lililowua mabosi wake wa zamani.

Kipagwile alifunga bao hilo dakika ya 58 kwa shuti zuri baada ya kupokea pasi safi ya kiungo Frank Domayo, aliyegongeana vema na mshambuliaji Bernard Arthur, bao lililodumu hadi dakika 90 za mchezo huo zinamalizika.

Mabingwa hao watetezi wa kombe hilo, wangeweza kujipatia bao la mapema zaidi kama Bernard angeitumia vema krosi ya Yahya Zayd, dakika ya kwanza akiwa ndani ya eneo la hatari lakini aliupiga vibaya mpira kabla ya kuokolewa na mabeki.

Kama mwamuzi wa mchezo huo angekuwa makini angeweza kuizawadia penalti Azam FC dakika ya nne baada ya beki wa Simba, Asante Kwasi, kumwangusha kwa makusudi mshambuliaji Yahya Zayd, aliyekuwa kwenye harakati za kuipatia bao timu yake.

Hadi dakika 45 za kipindi cha kwanza zinamalizika, timu zote ziliweza kutoshana nguvu, ambapo kipindi cha pili Azam FC ilionekana kubadilika kiuchezaji tofauti na ilivyouanza mchezo huo awali, hasa baada kuingia kiungoa Domayo dakika ya 56 kuchukua nafasi ya Zayd aliyeumia.

Domayo aliweza kumtengenezea pasi nzuri ya bao Kipagwile na kuifanya Azam FC kuendeleza mbio za kutetea ubingwa wake, na sasa ikisubiria kucheza hatua ya nusu fainali na moja ya timu kati ya Yanga au Singida United Januari 10 mwaka huu.

Kipa wa Azam FC, Razak Abalora, amechaguliwa kuwa mchezaji bora wa mchezo huo baada ya kuonyesha kiwango kikubwa akiokoa michomo mingi ya Simba na kuwanyima nafasi ya kusawazisha bao hilo.

Ni wazi sasa Simba inaendeleza uteja kwa Azam FC kwa mwaka wa pili mfululizo, ambapo mara ya mwisho kukutana kwenye fainali ya michuano hiyo mwaka jana, Azam FC iliibuka kidedea kwa ushindi wa bao 1-0, lililofungwa kiustadi kwa shuti la mbali na nahodha Himid Mao ‘Ninja’.

Kikosi cha Azam FC leo:

Razak Abalora, Himid Mao (C), Bruce Kangwa, Agrey Moris, Yakubu Mohammed, Stephan Kingue, Joseph Mahundi, Salmin Hoza/Abdallah Kheri dk 90, Yahya Zayd/Frank Domayo dk 56, Bernard Arthur/Paul Peter dk 89, Idd Kipagwile/Braison Raphael dk 78