BAADA ya kucheza mechi saba (sawa na dakika 630) mfululizo za Kombe la Mapinduzi bila kuruhusu wavu wake kuguswa, Azam FC imeshindwa kuendeleza rekodi hiyo baada ya kufungwa bao 1-0 dhidi ya URA ya Uganda, mchezo uliofanyika Uwanja wa Amaan, Zanzibar.

Bao pekee la URA limefungwa na Nicholas Kagaba dakika ya 33, lililodumu hadi dakika 90 za mchezo huo zinamalizika, licha ya Azam FC kufanya mabadiliko kadhaa ya kuwaingiza Enock Atta, Salmin Hoza, Shaaban Idd, Bernard Arthur na Hamimu Karim.

Azam FC kwa matokeo hayo imeshuka kwa nafasi moja hadi ya pili ikibakiwa na pointi sita huku URA ikiongoza Kundi A kwa pointi saba, Simba ni ya tatu ikiwa na pointi nne sawa na Mwenge huku Jamhuri ikishika mkia ikiwa na pointi moja tu.

Ili Azam FC ifuzu kwa hatua ya nusu fainali inatakiwa kushinda au sare kwenye mchezo wa kesho dhidi ya Simba, utakaofanyika Uwanja wa Amaan, Zanzibar 2.15 usiku.

Kikosi cha Azam FC leo:

Benedict Haule, Swaleh Abdallah, Bruce Kangwa, Abdallah Kheri, Yakubu Mohammed, Braison Raphael/Hamimu Karim dk 67, Masoud Abdallah/Enock Atta dk 46, Frank Domayo, Paul Peter/Shaaban Idd dk 59, Yahya Zayd/Bernard Arthur dk 46, Idd Kipagwile/Salmin Hoza dk 46