NI ushindi tu! Unaweza kuielezea hivyo gia waliyoingia nayo Azam FC kwenye michuano ya Kombe la Mapinduzi ikiendeleza mauaji baada ya kuichapa Jamhuri ya Pemba mabao 4-0, mchezo uliofanyika Uwanja wa Amaan usiku huu.

Ushindi huo umeifanya Azam FC kupanda kileleni mwa Kundi A baada ya kufikisha pointi sita, na hivi sasa ikihitaji pointi tatu tu kwenye mechi mbili zilizobakia ili kuweza kufuzu kwa hatua ya nusu fainali ya michuano hiyo.

Ilibidi Azam FC isubiri hadi dakika ya 26 kuweza kuandika bao la uongozi lililofungwa na mshambuliaji mpya Bernard Arthur, aliyemalizia krosi safi ya chini iliyopigwa na Bruce Kangwa, aliyetanguliziwa mpira wa adhabu ndogo na Yahya Zayd.

Jamhuri ililazimika kucheza pungufu kwa takribani dakika 48 za mchezo huo baada ya beki wao Abdul Mahfudh, kuonyeshwa kadi nyekundu iliyotokana na kadi mbili za njano alipomfanyia madhambi ya makusudi winga Joseph Mahundi.

Hadi kipindi cha kwanza kinamalizika, Azam FC ilienda mapumziko ikiwa mbele kwa bao hilo, ambapo ilirejea kipindi cha pili kwa kasi kubwa zaidi na kujipatia mabao mengine matatu yaliyohitimisha ushindi huo mnono.

Kiungo Salmin Hoza, aliyechaguliwa kuwa Mchezaji Bora wa mchezo huo aliipatia bao la pili Azam FC dakika ya 47 baada ya kupiga shuti kali nje kidogo ya eneo la 18, lilomshinda kipa wa Jamhuri.

Mshambuliaji kinda anayekuja kwa kasi, Yahya Zayd, alitupia bao la tatu kwa upande wa Azam FC kwa mpira wa adhabu ndogo ya moja kwa moja iliyomshinda kipa, aliyepangulia mpira nyavuni.

Aliyehitimisha dozi hiyo alikuwa ni mshambuliaji hatari kinda wa timu hiyo, Paul Peter, aliyeingia dakika ya 58 kuchukua nafasi ya Arthur na kuipatia bao la nne alilofunga kiufundi baada ya kumiliki mpira mbele ya mabeki na kugeuka na mpira kabla ya kupiga shuti lililotinga kimiani.

Mara baada ya mchezo huo, kikosi cha Azam FC kitamalizia mechi zake za mwisho za Kundi A kwa kukipiga na URA ya Uganda keshokutwa Ijumaa saa 10.30 jioni kabla ya kesho yake kukipiga na Simba saa 2.15 usiku.

Hadi sasa wakati michuano hiyo, inaendelea Azam FC ndio timu pekee ambayo haijaruhusu wavu wake kuguswa katika mechi mbili ilizocheza ya kwanza ikiichapa Mwenge mabao 2-0, yote yakifungwa na Peter, ambaye hadi sasa ndiye kinara wa ufungaji akiwa na mabao matatu.

Kikosi cha Azam FC leo:

Razak Abalora, Swaleh Abdallah/Abdul Omary dk 77, Bruce Kangwa, Agrey Moris/Oscar Masai dk 82, Yakubu Mohammed/Abdallah Kheri dk 53, Stephan Kingue, Joseph Mahundi, Salmin Hoza, Yahya Zayd/Shaaban Idd dk 77, Bernard Arthur/Paul Peter dk 58, Enock Atta