KLABU Bingwa ya Afrika Mashariki na Kati, Azam FC, inatarajia kutupa karata yake ya pili ya michuano ya Kombe la Mapinduzi kwa kukipiga dhidi ya Jamhuri ya Pemba, mchezo utakaofanyika Uwanja wa Amaan, Zanzibar kesho Jumatano saa 10.30 jioni.

Azam FC ambayo ni bingwa mtetezi wa michuano hiyo, ilianza vema kampeni yake ya kulitetea baada ya kuichapa Mwenge mabao 2-0 kwenye mechi yake ya kwanza ya michuano hiyo, yaliyofungwa na mshambuliaji kinda Paul Peter.

Kuelekea mchezo kikosi cha Azam FC mpaka sasa kinashika nafasi ya pili kwenye Kundi A kikiwa na pointi tatu kikizidiwa pointi moja na Mwenge yenye pointi nne kufuatia sare ya bao 1-1 dhidi ya Simba, lakini ikiwa mbele mechi mbili za kucheza dhidi ya matajiri hao.

Katika mchezo wa kwanza, benchi la ufundi liliwatuamia wachezaji wengi chipukizi na wale wasiopata nafasi ya kucheza mara kwa mara, lakini halikuharibika jambo kutokana na ubora wa kikosi cha Azam FC na kupata ushindi huo mnono.

Mara baada ya mazoezi ya mwisho leo jioni kuelekea mchezo huo, Kocha Mkuu wa Azam FC, Aristica Cioaba, alisema kuwa wamejipanga kupata ushindi dhidi ya timu hiyo kutoka Pemba huku akidokeza kuwa watachukulia uzito kila mechi ili kuweza kushinda na kutetea ubingwa.

“Mechi hii nitawapa nafasi wachezaji ambao hawakucheza mechi ya kwanza lakini nitapenda kuwaona wakionyesha umakini na kuuchukulia uzito mchezo kama kilivyocheza kikosi kilichocheza mechi ya kwanza, tumekuja huku kwa kazi moja tu kushinda mechi zote na kutetea ubingwa.

“Nilifurahishwa sana na hali ya umakini ulioonyeshwa na wachezaji kwenye mechi ya kwanza, napenda kumuona kila mchezaji atakayecheza basi aiheshimu nembo ya klabu kwa kupambana na kupata matokeo, tutakachofanya ni kuhakikisha tunashinda kila mchezo ili kubeba tena kombe hili,” alisema Cioaba.

Alisema jambo la kufurahisha ni kikosi hicho kutokuwa na majeruhi wapya isipokuwa mshambuliaji Mbaraka Yusuph, ambaye bado anaendelea na mapumziko huku akidai kuwa wachezaji wengine winga Joseph Kimwaga, beki David Mwantika na nahodha Himid Mao ‘Ninja’,  hali zao zinaendelea kutengamaa.

Mara baada ya kumaliza mchezo huo, Azam FC itabakisha mechi mbili za mwisho za Kundi A, mechi ya kwanza ikitarajia kucheza Januari 5 dhidi ya URA ya Uganda saa 10.30 jioni kabla ya siku inayofuata kukipiga dhidi ya Simba saa 2.15 usiku.