MSHAMBULIAJI kinda wa Azam FC, Paul Peter, amemwambia kocha wa timu hiyo Aristica Cioaba, kuwa hatojuta kwa uamuzi wake wa kuendelea kumuamini kwenye kikosi hicho huku akimuahidi kuendelea kufunga kila anapompa nafasi.

Kauli ya Peter imekuja muda mchache mara baada ya kufunga mabao mawili yaliyoipa ushindi wa mabao 2-0 Azam FC dhidi ya Mwenge usiku wa kuamkia leo katika mchezo wake wa kwanza wa Kundi A la michuano ya Kombe la Mapinduzi.

Mshambuliaji huyo aliyeko kwenye kikosi cha timu ya Taifa ya Vijana chini ya umri wa miaka 20 (Ngorongoro Heroes), mpaka sasa tokea apandishwe timu kubwa Oktoba mwaka jana ameshafunga mabao sita, matatu kwenye mashindano na mengine yaliyobakia katika mechi za kirafiki.

Alifunga bao la kwanza na kuipa Azam FC pointi moja kwenye mchezo wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara (VPL) dhidi ya Singida United ulioisha kwa sare ya bao 1-1, akafunga jingine katika mchezo wa kirafiki dhidi ya Mvuvumwa, ambao Azam FC ilishinda mabao 8-1.

Mengine mawili alifunga katika mchezo mwingine wa kirafiki wakati Azam FC ikiichapa Polisi Tanzania mabao 3-1 huku jana akitupia mengine mawili dhidi ya Mwenge inayotokea Kisiwani Pemba, Zanzibar.

Akizungumza na mtandao rasmi wa klabu www.azamfc.co.tz Peter alisema siri ya kufanya kwake vizuri ni mazoezi tu na kusikiliza maelekezo anayopewa na kocha.

“Najisikia vizuri sana kuifungia Azam FC mabao hayo, mashindano ni mazuri nahisi huko mbeleni yatakuwa magumu zaidi kwa sababu kuna timu nzuri tutakutana nazo huko mbele lakini tutahakikisha tunapambana na kutetea ubingwa wetu,” alisema.

Alisema kwa sasa haangalii hata kidogo kuwania kiatu cha ufungaji bora wa michuano hiyo badala yake anachopigania ni kushirikiana na wachezaji wenzake kufanya vizuri kwa ajili ya kutetea ubingwa walioutwaa mwaka jana kwa kuifunga Simba bao 1-0.

“Naamini tutatetea taji letu, mashabiki watarajie mazuri kutoka kwangu kama nilivyowaahidi mwanzo nilipoanza kucheza, nafurahi sana kwa sasa kucheza na wachezaji wazoefu kwani wananipa morali ya kujiamini wakati ninapocheza, ninapokosea wananirekebisha tunasaidiana, namshukuru kocha kwa kuniamini namuahidia nitaendelea kutumia vema nafasi anazonipa na kuendelea kufunga,” alisema.

Mara baada ya kumaliza mchezo huo wa kwanza, katika mchezo wa pili wa michuano hiyo Azam FC itakipiga dhidi Jamhuri ya Pemba, mtanange utakaopigwa keshokutwa Jumatano saa 10.30 jioni.