KLABU Bingwa ya Afrika Mashariki na Kati, Azam FC, imeanza vema harakati za kutetea ubingwa wa Kombe la Mapinduzi baada ya kuinyuka Mwenge mabao 2-0, mchezo uliofanyika usiku huu kwenye Uwanja wa Amaan, Zanzibar.

Kwa ushindi huo, Azam FC imekaa kileleni mwa Kundi A ikiwa na pointi tatu sawa na Mwenge, ambayo ilipata ushindi kwenye mchezo wa kwanza dhidi ya Jamhuri, zote zikiwa ni timu kutoka Pemba.

Benchi la ufundi la Azam FC liliutumia mchezo huo wa kwanza kuwapa nafasi wachezaji ambao hawakupata nafasi ya kucheza kwenye mchezo uliopita wa ligi dhidi ya Stand United pamoja na wale waliocheza dakika chache.

Mshambuliaji chipukizi wa timu hiyo, Paul Peter, ndiye aliyeibuka shujaa baada ya kufunga mabao yote mawili la kwanza akitupia dakika ya 41 baada ya kazi nzuri iliyofanywa na mshambuliaji Bernard Arthur, aliyepiga shuti lililopanguliwa na kipa kabla ya mfungaji kuuwahi mpira na kumalizia.

Peter aliyechaguliwa kuwa mchezaji bora wa mchezo huo, alifunga bao la pili dakika ya 62 akimalizia pia kwa shuti baada ya kukutana na mpira uliotemwa na kipa kufuatia shuti lililopigwa na Idd Kipagwile.

Baada ya mchezo huo, Azam FC itashuka tena dimbani Jumatano ijayo kuvaana na Jamhuri ya Pemba, mchezo utakaofanyika Uwanja wa Amaan saa 10.30 jioni.

Kikosi cha Azam FC leo:

Mwadini Ally, Swaleh Abdallah, Hamimu Karim, David Mwantika/Oscar Masai dk 46, Yakubu Mohammed, Braison Raphael, Masoud Abdallah/Shaaban Idd dk 84, Frank Domayo/Enock Atta dk 76, Bernard Arthur, Paul Peter/Wazir Junior dk 68, Idd Kipagwile