KIKOSI cha Klabu Bingwa ya Afrika Mashariki na Kati, Azam FC, tayari kimeshakanyaga kwenye ardhi ya visiwani Zanzibar, ambapo kesho Jumapili inatarajia kuanza kutetea taji lake la Mapinduzi Cup kwa kumenyana na Mwenge katika Uwanja wa Amaan saa 10.30 jioni.

Mabingwa hao wametua mchana visiwani humo wakiwa na kikosi chote kamili, wamefikia katika Hoteli ya kifahari ya Mtoni Marine, yenye utulivu mkubwa.

Katika kuonyesha kuwa imedhamiria kufanya kweli, Azam FC mara baada ya kuwasili Zanzibar haijapata muda mrefu wa kumpumzika baada ya jioni ya leo kufanya mazoezi tayari kujiweka sawa kuelekea mchezo wa kesho dhidi ya timu hiyo kutoka Pemba.

Kutokana na Azam FC kucheza mchezo wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara (VPL) dhidi ya Stand United jana na kushinda mabao 3-0, huenda benchi la ufundi likawapumzisha baadhi ya wachezaji waliocheza asilimia kubwa ya mchezo huo ili kutowachosha zaidi.

Mwaka huu Azam FC ilionyesha umwamba ilipotwaa taji hilo kwa mara ya tatu ikiifunga Simba bao 1-0, mbali na kujiongezea rekodi hiyo pia iliweza kubeba taji bila kuruhusu wavu wake kuguswa kwa mechi zote tano ilizocheza hadi hatua ya fainali.

Azam FC imejidhatiti kuweza kutetea ubingwa huo na ndio maana imeshusha kikosi chote kamili kwa ajili ya michuano hiyo, kikiwa pia na wachezaji wanne vijana ambao ni mabeki Oscar Masai, Abdul Omary, Ramadhan Mohamed na mshambuliaji Paul Peter.